Habari Mseto

Rais ataka KDF wachangie zaidi ustawi wa nchi

September 11th, 2019 1 min read

Na PSCU

RAIS Uhuru Kenyatta ametoa wito kwa Jeshi la Ulinzi wa Kenya (KDF) kushiriki moja kwa moja katika kufanikisha ustawi wa Kenya.

Rais jana alisema ustawi wa nchi hii unategemea mazingira ya amani na usalama unaotolewa na jeshi pamoja na asasi nyingine husika za usalama na ulinzi.

“Kwa misingi hiyo, ninafurahi kutambua juhudi ambazo Wizara ya Ulinzi inatekeleza kupanua ustawi wa kiviwanda katika shughuli za kijeshi,” akasema.

Rais Kenyatta alikuwa akizungumza katika Chuo cha Mafunzo kwa makurutu wa Jeshi Eldoret alipoongoza sherehe za kufuzu kwao.

Mbali na mipaka ya Kenya, Jeshi la Ulinzi la Kenya pia limekuwa mstari wa mbele katika udumishaji wa amani ya kanda na ya Kimataifa kama mchango wa nchi hii katika kuimarisha mazingira thabiti ulimwenguni.

Rais alisema kwamba jeshi la KDF litaendelea kuunga mkono harakati za kuleta amani na uthabiti nchini Somalia chini ya kikosi cha Muungano wa Afrika cha kuhifadhi amani nchini humo AMISOM.

Wakati wa sherehe hiyo, Rais Kenyatta aliwakabidhi tuzo makurutu walioibuka washindi katika nyanja mbalimbali za mafunzo.

Kurutu aliyeibuka bora katika kila nyanja ya mafunzo alikuwa Becky Juma, naye Paul Nduta alichukua nafasi ya pili huku John Tsome akiwa wa tatu. Quintine Indeche alichukua nafasi ya kurutu bora zaidi katika mafunzo ya mapambano ya ulengaji shabaha.

Msimamizi wa Chuo hicho cha Mafunzo cha Eldoret, Brig. Peter Njiru alisema wanajeshi hao waliofuzu watapelekwa kuhudumu katika vikosi mbali mbali vya kijeshi nchini.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na wakuu wa jeshi wakiongozwa na Mkuu wa Majeshi Jemedari Samson Mwathethe. Waziri wa Ulinzi Raychelle Omamo na maafisa wengine wakuu serikalini pia walihudhuria sherehe hiyo.