Habari MsetoSiasa

Rais ataka mzozo kuhusu ugavi wa fedha utatuliwe

August 15th, 2019 2 min read

PHYLLIS MUSASIA, DAVID MUCHUI na PSCU

RAIS Uhuru Kenyatta ametoa wito kwa Bunge la Kitaifa na Seneti kukomesha mzozo kuhusu Mswada wa Ugavi wa Mapato wa mwaka huu ili kuwezesha serikali za kaunti kupewa fedha.

Alisema fedha zikicheleweshwa zaidi, Wakenya watanyimwa huduma muhimu wanazohitaji.

Hata hivyo, Rais aliwakumbusha wabunge kwamba, serikali haina fedha za kutosha kuongeza kaunti , akisema Serikali Kuu imekuwa ikigawia kaunti pesa kupita kiwango kilichowekwa katika katiba.

“Katiba inasema tugawie kaunti kiasi kisichopungua aslimia 15. Katika kipindi cha mwaka mmoja, niliongeza kiwango hicho hadi aslimia 30. Kwa nini msipitishe mswada huo ili watu wapate huduma na kuafikia makubaliano ili tutoe fedha kwa serikali za kaunti?” akasema Rais.

Rais Kenyatta alisema viongozi pia wanafaa kubadili mawazo na ufahamu wao kuhusu ugatuzi kwa sababu mfumo huo wa utawala haumanishi mashindano kati ya ngazi hizo mbili za serikali.

“Hii ni mifumo miwili ya serikali inayosaidiana kutoa huduma kwa wananchi,” akasema Rais.

Mwanasheria Mkuu alitarajiwa kutoa mwelekeo wa kisheria jana ikiwa Wizara ya Fedha inaweza kutoa fedha kwa kaunti bila kusubiri mswada upitishwe bungeni. Hakuwa amefanya hivyo kufikia wakati wa kuenda mitamboni jana.

Huku hayo yakijiri, baadhi ya wafanyakazi wa kaunti, hasa wauguzi waliendelea kurejea kazini jana baada ya kuafikiana na kaunti zao.

Katika Kaunti ya Meru, wahudumu wa afya waliamua kurejea kazini baada ya kuahidiwa kwamba watalipwa mishahara yao ifikapo Jumanne ijayo.

Uamuzi huo ulitolewa baada ya mkutano kufanywa kati ya wawakilishi wao na maafisa wa kaunti, wakiongozwa na Gavana Kiraitu Murungi.

Chama cha Wafanyakazi wa Kaunti (KCGWU) kilisema wafanyakazi wa kaunti 21 walikuwa hawajapokea mishahara ya Julai.

Madaktari na wauguzi katika kaunti ya Nakuru walirejea kazini jana lakini wakaipa serikali ya kaunti makataa ya hadi Ijumaa wiki hii kulipwa mishahara yao.

Wakiongozwa na Dkt Davji Attela ambaye ni katibu mkuu wa chama cha madaktari katika eneo la South Rift, wauguzi hao walisema hawatakuwa na budi kususia kazi ifikapo Ijumaa iwapo ahadi waliopewa haitatimizwa.

“Nimewasihii madaktari pamoja na wauguzi kuendela na kazi hadi Ijumaa kwa sababu hiyo ndiyo siku ambayo serikali ya kaunti imeahidi kuwalipa,” akasema Dkt Attela.

Mnamo Jumanne, shughuli zilitatizika katika hospitali ya Nakuru Level Five huku baadhi ya wagonjwa wakililazimika kurudi nyumbani bila kuhudumiwa.

Uchunguzi wa Taifa Leo katika hospitali hiyo Jumatano ulibaini foleni ndefu za wagonjwa waliorejea baada ya kukosa matibabu mnamo Jumanne.

Bi Jane Wangui alisema kuwa walilazimika kumrejesha mwanawe nyumbani baada ya kufika hospitali humo na kusubiri masaa kadha bila kuhudumiwa.

“Mwanangu ni mgonjwa, ana joto jingi na inapofika usiku hali, halali, analia tu,” akaeleza Bi Wangui ambaye alitazamia mwanawe angehudumiwa.

Mwanamume mwingine aliyeonekana kulemewa hakuruhusiwa kwenda mbele ya wenzake waliokuwa kwenye foleni ya kumuona daktari.