Habari Mseto

Rais atakiwa aingilie kati kunusuru sekta ya majanichai

November 8th, 2019 2 min read

Na IRENE MUGO  na CHARLES WASONGA

KAMATI ya Seneti kuhusu Kilimo imemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuunda jopokazi la kudadisi malalamishi ya wakulima katika sekta ya majanichai dhidi ya Mamlaka ya Ustawi wa Majanichai Nchini (KTDA).

Wanachama wa kamati hiyo wanasema jopokazi hili litachunguza madai kwamba mamlaka hiyo huwekeza fedha za wakulima katika miradi feki ambayo haileti faida yoyote kwa wakulima.

Wakati wa vikao vya kukusanya maoni na mapendekezo kutoka kwa umma na kamati hiyo katika kaunti sita ambako majani chai hukuzwa kwa wingi, wakulima walilalamikia ukosefu wa uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa KTDA.

Kamati hiyo iliamb ia kuwa wakulima wa majani chao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali katika jitihada zao za kuchuma mapato kutokana na kilimo cha zao hili.

Changamoto zinazowakabili wakulima wa majanichai ni kama vile bei duni ya majanichai shambani, ukosefu wa hudumu za wataalamu wa masuala ya kilimo, ukosefu wa mikopo na kutoshirikishwa kwa wakulima katika majukwaa ya kufanya maamuzi.

Katika kaunti ya Murang’a, wakulima walisema serikali ya kaunti imekarabati barabara katika maeneo kunakokuzwa kahawa na kuacha nje maeneo yenye mashamba ya majani chai.

Aidha, walilalamimkia kuwa Bodi ya Majanichai na Taasisi ya Utafiti kuhusu zao hilo (TRI) zililemazwa wakati Mamlaka ya Kilimo na Chakula (AFA) ilibuniwa, hali ambayo imefanya idara ya chai katika Wizara ya Kilimo kuwa butu.

“Tulipendekeza kuwa zao la majanichai liondolewe kutoka AFA na badala yake bodi mahususi ya kulisimamia liundwe,” ikasema kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Embu Njeru Ndwiga katika ripoti yake.

Wakulima pia walilalamika kuwa kuna mwingiliano wa kimajukumu kati ya serikali ya kitaifa na zile za kaunti na KTDA kuhusiana na usimamizi wa sekta ya majanichai. Wanataka majukumu ya asasi hizi yabainishwe.

Wakulima pia wanataka wauziwe mbolea kwa bei ya chini na bei ya majanichai mabichi shambani iongezwe.

“Kila mkulima anapasa kulipwa Sh20 kwa kilo ya majanichai mabichi na baada ya miezi sita alipwe bonasi ya Sh50 kwa kilo badala ya Sh5,” akasema mkulima mmoja kutoka Embu.

Mkulima huyo aliongeza kuwa mwishoni mwa mwaka mkulima anastahili kulipwa Sh20 kwa kilo na kufanya jumla ya malipo yake kwa mwaka kuwa Sh120 kwa kilo ya majanichai mabichi.