Habari za Kitaifa

Rais atangaza mikakati ya kuleta shibe kubwa Kenya

June 2nd, 2024 2 min read

NA BENSON MATHEKA

RAIS William Ruto amesema serikali yake ina mikakati ya kupunguza njaa na umasikini nchini kupitia kilimo na kuimarisha uchumi.

Akisisitiza umuhimu wa kilimo kwa uchumi wa nchi, Rais Ruto alisema serikali yake haitaacha nyuma sehemu ya jamii au eneo lolote katika kupiga vita uhaba wa chakula na umasikini.

“Hakuna anayefaa kudharau maisha au kazi ya mwingine na hakuna anayepaswa kuhisi kudharauliwa kwa sababu ya kazi yake. Uchumi wetu unategemea kila aina ya huduma na kazi. Kuanzia kwa usagaji wa miwa, mtama na mawele hadi kuchakata pamba na kuchoma kahawa katika nchi hii, sekta yetu ya kilimo inaendelea kuwasha injini yenye nguvu ya mageuzi ya kiuchumi na kufanya nchi hii tukufu kujitoshelesha kwa chakula, na kushindana kimataifa kibiashara,” Rais alisema akihutubia Wakenya katika maadhimisho ya 61 ya Madaraka Dei.

Akisema kilimo kinachangia moja kwa moja asilimia 25 ya pato la taifa, na kupiga jeki mihimili mingine ya uchumi vikiwemo viwanda kwa asilimia 27, kuajiri zaidi ya asilimia 40 ya Wakenya, kiongozi wa nchi alisema kwamba serikali imeanza mageuzi ya kutumia sekta hiyo kuimarisha mapato ya Wakenya, kupunguza njaaa, kupiga vita umasikini.

“Tutapunguza njaa, kupiga vita umasikini na kuimarisha mapato na afya ya Wakenya. Hasa ninafurahia kuwa kilimo na utoshelevu wa chakula ndiyo mada ya sherehe za mwaka huu,” alisema Rais.

Alipongeza wakulima wa mashamba madogo kwa kutia bidii kuzalisha chakula licha ya changamoto nyingi.

“Tunaelewa, tunawatambua na kuwathamini,” alisema.

Ili kuwasaidia, Rais alisema serikali imeshirikiana na wakulima na wadau wengine katika mfumo wa thamani wa kilimo, wakiwemo wasambazaji na watengenzaji pembejeo kubadilisha kilimo cha wakulima wa mashamba madogo kuafikia utoshelevu wa chakula nchini.

“Hii imewezekana kupitia usaidizi katika mifumo muhimu ya thamani kama mahindi, mifugo, chai, mafuta ya kupikia, korosho, alizeti, parachichi na makadamia,” alisema.

Ili kuimarisha uwezo wa kushirikisha uzalishaji wa kilimo na kutoa huduma kwa ufanisi, serikali imeanzisha mfumo wa data za wakulima na wajasiriamali wa kilimo.

Alisema mpango wa mbolea ya ruzuku, lishe ya mifugo na mbegu zilizodhinishwa umesaidia wakulima kuimarisha uzalishaji na kwamba mipango inaendelea kuimairisha uzalishaji wa kahawa kutoka tani 50,000 hadi tani 102,000 kufikia 2027.

Rais alitangaza kuwa serikali itafuta madeni ya Sh6.9 bilioni yanayodaiwa wakulima kupitia vyama vya ushirika vya kahawa.

Katika mfumo wa thamani wa mafuta ya kupikia, Rais alitangaza kuwa serikali ya kitaifa itashirikiana na za kaunti kupiga jeki uzalishaji wa alizeti, mafuta ya mawese na kanola.

“Mpango wetu wa kuongeza uzalishaji wa pamba unaendelea. Tunaendelea kupanua kilimo cha pamba kutoka ekari 9,300 mwaka wa 2022 hadi 41,000 mwaka wa 2023,” alisema.

Serikali inalenga kaunti za Busia, Meru, Makueni, Kitui na Machakos kuongeza kilimo cha pamba.

Ili kuongeza thamani bidhaa za mifugo, serikali itaweka mikakati ya kuinua mapato ya wakulima kutoka Sh15 bilioni hadi Sh120 bilioni kwa mwaka kwa kuanzisha viwanda vya ngozi Ewaso Ng’iro kwa gharama ya Sh200 milioni na Kenanie, Machakos ambacho asilimia 85 imekamilika.

“Tumejitolea kuimarisha uzalishaji wa maziwa kutoka lita bilioni 5.1 hadi bilioni 10 kwa mwaka kufikia 2027,” alisema Rais.