Habari Mseto

Rais ateua kijana baada ya kushutumiwa kwa kuendeleza mtindo wa kuteua wazee

October 24th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

HATIMAYE Rais Uhuru Kenyatta ameteua kijana katika wadhifa wa umma baada ya wananchi kuisuta serikali yake kutokana na mtindo wake wa kuteua wazee katika nyadhifa hizo.

Mnamo Jumanne, Oktoba 22, 2019, Rais alimteua Peris Wambui Nyutu kuwa mwanachama wa Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC).

Bi Nyutu, 28, alisomea Uanasheria katika Chuo Kikuu cha Nairobi na aliwahi kuwa mwanachama wa Kamati Kuu ya Chama cha Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi (SoNU).

Vilevile, amewahi kuhudumu kama mwanachama wa Bodi ya Kitaifa ya Unyunyiziaji (NIB).

Na mnamo 2018 alikuwa miongoni mwa watu ambao Rais Uhuru Kenyatta aliwapa tuzo ya taadhima ya The Order of the Grand Warrior of Kenya.

Na wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu wa 2017 Bi Wambui Nyutu alikuwa mmoja wa viongozi wa kundi la vijana maarufu kama ‘Warembo na UhuRuto’ walioshiriki kampeni za kupigia debe kuchaguliwa tena kwa Rais Kenyatta.

Uteuzi huo unajiri wiki moja baada ya uteuzi wa aliyekuwa mbunge wa Othaya Mary Wambui kuwa mwenyekiti wa Mamlaka ya Kitaifa ya Uajiri (NEA) kuibua pingamizi kubwa miongoni mwa Wakenya.

Wengi walidai kuwa wadhifa huo, alifaa kupewa Mkenya mwingine, mwenye umri mdogo na wala sio Bi Wambui mwenye umri wa miaka 71.

Na Jumatano uteuzi huo ulisimamishwa na Mahakama ya Kusikiza kesi za Ajira na Masuala ya Leba kufuatia kesi iliyowasilishwa na Seneta wa Nairobi Johnston Sakaja.

Atoa pongezi

Jumatano Bi Nyutu alichangamkia kuteuliwa kwake na kumpongeza Rais Kenyatta kwa kutunukia heshima ya kuhudumu katika tume hiyo.

“Kwanza namshukuru Rais Uhuru Kenyatta kwa kunipendekeza kuwa kamishna katika NCIC. Kwa unyenyekevu namshukuru kwa heshima hii. Asant eRais,” akasema kwenye ujumbe alioweka katika ukurasa wa akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Facebook.

Akaongeza: “Nitajitahidi niwezavyo kwa heshima ya vijana wa taifa hili.”

Alielezea matumaini yake kwamba Bunge litaidhinishwa kuteuliwa kwake.

Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Murang’a Sabina Chege ni miongoni kwa wanasiasa waliompongeza Bi Nyutu kwa uteuzi huo.

“Pongezi msichana kutoka kwetu Murang’a, kiongozi wa vijana na wakili Wambui Nyutu kufuatia kuteuliwa kwake na Rais Uhuru Kenyatta kuwa kamishna wa NCIC. Kwa niaba ya watu wa Murang’a nasema kongole,” Mhe Chege akasema katika ujumbe wake.

Tume ya NCIC ilibuniwa mnamo 2008 kuendeleza umoja wa kitaifa kwa kuchunguza masuala yanayosababisha ubaguzi wa kikabila, ugavi usiofaa wa rasilimali za umma na nafasi za ajira, kuendesha kampeni ya kuzima uchochozi wa chuki, kati ya maovu mengine ambayo huathiri utangamano wa kitaifa.