Habari

Rais ateua rasmi mwenyekiti na makamishna wapya wa NLC

October 3rd, 2019 2 min read

RAIS Uhuru Kenyya ameteua rasmi wanachama wapya wa Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC).

Kwa mujibu wa tangazo lililochapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali, Rais alimteua Wakili Gershom Otachi kuwa mwenyekiti wa tume hiyo kwa kipindi cha miaka sita kuchukua nafasi ya Profesa Mohammed Swazuri ambaye muda wake wa kuhudumu ulikamilika mnamo Aprili 2019.

Bw Otachi ambaye ni mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Ustawi wa Kawi inayotokana na Mvuke (GDA) aliwahi kuhudumu kama wakili wa Wakenya sita waliofikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa tuhuma za kuchochea na kufadhili ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007.

Baadhi ya washtakiwa hao walikuwa ni Rais Kenyatta na naibu wake William Ruto ambao kesi zao zilikosa kuendelea baada ya mashahidi kujiondoa.

Rais Kenyatta pia aliwateua watu wanane ambao majina yao yaliidhinishwa Jumanne na Bunge kuwa wanachama wa tume hiyo ambayo itashughulikia masuala ya ardhi kwa ushirikiano na Wizara ya Ardhi.

Walioteuliwa kuwa wanachama wa tume hiyo ni aliyekuwa Mbunge wa Nyeri Mjini Esther Murugi Mathenge, aliyekuwa Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Egerton Profesa James K. Tuitoek, Bi Getrude Nduku Nguku, Bw Reginald Okumu, Bi Hubbie Hussein Al Haji na Bw Alister Murimi Mutungi.

Wengine ni aliyekuwa Waziri wa Leba Samuel Kazungu Kambi na aliyekuwa Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Isiolo, Bi Tiya Galgalo.

Tangazo hilo kwenye gazeti rasmi la serikali lilijiri siku moja baada ya bunge la kitaifa kuifanyia marekebisho ripoti ya Kamati ya Bunge kuhusu Ardhi kwa kujumuisha jina la Bi Galgalo dakika za mwisho baada ya awali kukatiliwa kwa msingi kwamba hakuwa ametimiza masharti ya ulipaji ushuru kwa kujaza fomu rasmi mnamo miaka ya 2017 na 2018.

Bunge pia lilitupilia mbali ripoti ya wabunge Owen Baya (Kilifi Kaskazini), Teddy Mwambire (Ganze) na Omar Mwingi (Changamwe) waliopinga uteuzi wa Bw Kambi wakidai hakuhitimu kimasomo na kimaadili kwa wadhifa huo.

Jopo la uteuzi lilipokea maombi kutoka kwa watu 117 waliotaka wadhifa wa mwenyekiti na watu 940 waliokuwa wakimezea mate nafasi nane za makamishna wa NLC.