Habari Mseto

Rais atoa hakikisho kuhusu KCSE na KCPE

August 20th, 2018 1 min read

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta amewahikishia watahiniwa wote wa mwaka huu kwamba mitihani ijayo ya kitaifa itakuwa salama pasina visa vya udanganyifu.

Alisema serikali imejitolea kuhakikisha kulinda hadhi na maadili katika sekta ya elimu nchini.

Rais Kenyatta aliwaambia watahaniwa na mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE) na wale wa mtihani wa darasa la nane (KCPE) kwamba mitihani ya mwaka huu itaendeshwa kwa njia salama akiwataka kujiandaa barabara.

“Ningetaka kuwahakikishieni kuwa mitahani ya mwaka huu italindwa zaidi hata kulipa ile ya miaka ya nyuma,” akasema.

Rais alisema hayo Ijumaa alipotumbuizwa na wanafunzi waliofanya vizuri katika Tamasha ya Kitaifa ya Musiki katika Ikulu ndogo ya Sagana, kaunti ya Nyeri.

Alisema alama ambazo kila mtahiniwa atapata zitatokana na bidii yao huku zikiakisi jinsi walivyojiandaa.

Rais Kenyatta aliwataka wanafunzi kudumisha nidhamu akisema sifa zao kimaadili ni muhimu zaidi kulipa alama ambazo watapata katika mitihani.

Washindi katika mashindano hayo walijumuisha timu 27 kutoka maeneo mbalimbali nchini ambao waliwalisha sanaa za uigizaji, nyimbo, densi za kitamaduni, simulizi kati ya fani mbalimbali zenye ubunifu mkubwa.