Rais awacheza kama Moi 2002

Rais awacheza kama Moi 2002

Na IBRAHIM ORUKO

MBINU anazotumia Rais Uhuru Kenyatta kuhusu siasa za urithi muda wake wa urais ukifika kikomo mwaka ujao, ni marudio ya hali ilivyokuwa mnamo 2002, Daniel Moi alipokaribia kuondoka madarakani.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa Murithi Mutiga, Rais Kenyatta yuko katika hali aliyokuwa marehemu Moi mnamo 2002, wakati kila aliyekuwa karibu naye alitarajia kuidhinishwa naye kuwa mrithi wake.

Kwa wakati huu hali ni sawa, ambapo kila mmoja wa vigogo wa siasa za kikabila anategea kutangazwa na Rais Kenyatta kuwa afaaye kuwa mrithi wake kwenye uchaguzi wa 2022.

“Rais Kenyatta yuko pale pale alipokuwa Moi kabla ya uchaguzi wa 2002. Kila mmoja wa wanasiasa wakuu anataka kutangazwa mrithi wa urais. Kutegea huku kumemsaidia rais kutawala kwa utulivu kwani kila mmoja anajipendekeza kwa kujifanya mwaminifu kwake. Lakini Uhuru anacheza mchezo hatari kwa sababu ni vigumu kuchezea watu kama Raila na Ruto kwa pamoja,” akasema Bw Mutiga.

Mnamo 2002, Moi aliwavunja moyo wengi wa wanasiasa waliokuwa wakitarajiwa kuteuliwa kupeperusha bendera ya Kanu kwa kuwapuuza waliokuwa na uzoefu wa siasa kama Raila Odinga, aliyekuwa makamu wake George Saitoti, Kalonzo Musyoka na Musalia Mudavadi, na badala yake akatoa baraka zake kwa Bw Kenyatta, ambaye wakati huo alikuwa limbukeni kisiasa.

Hatua hiyo iliwafanya wengi wao kutoroka Kanu na kuungana na Mwai Kibaki, Kijana Wamalwa na Charity Ngilu katika chama cha Narc, ambacho kilishinda uchaguzi huo kwa kura nyingi.

Bw Mutiga, ambaye ni Mkurugenzi wa Mipango eneo la Upembe wa Afrika katika shirika la International Crisis Group, asema bahati anayoweza kuwa nayo Rais Kenyatta ni iwapo Bw Odinga ataamua kujiondoa kwenye kinyang’anyiro cha urais mwaka ujao.

Mnamo 2002, kuondoka kwa Bw Odinga kwenye mrengo wa Kanu na kutangaza kumwidhinisha Mzee Kibaki, kulichangia pakubwa katika kushindwa kwa Bw Kenyatta.

Kati ya wanasiasa ambao wanaomba kupata baraka za Rais Kenyatta kama wafaao kumrithi ni Bw Odinga, Musyoka, Mudavadi (ANC), Gideon Moi (Kanu) na Moses Wetangula wa Ford-Kenya.

Pia kuna Charity Ngilu, magavana Hassan Joho (Mombasa) na Wycliffe Oparanya (Kakamega) na Mukhisa Kituyi.

Naibu Rais William Ruto kwa upande wake anaonekana kukubali kuwa hayuko kwenye hesabu za urithi za bosi wake.

Lakini baadhi ya wachanganuzi wanasema rais hajamfungia milango kabisa naibu wake, kwani huenda akamhitaji iwapo Bw Odinga atakosa kusakata ngoma anavyotaka rais.

Katika kile kinawatia kiwewe vigogo wote walio na ndoto za kuidhinishwa na rais kuwa wafaao kuwa warithi wake, Rais Kenyatta amekuwa akiwaweka wote katika hali ya mshikemshike kwa kukosa kujitokeza wazi kuonyesha mahali roho yake imo kikamilifu.

Bw Odinga na wandani tayari wameanza kuingia kiwewe baada ya Rais Kenyatta kuanza kuegemea mrengo wa kundi la One Kenya Alliance unaojumuisha Moi, Mudavadi, Kalonzo, Ngilu na Wetangula.

Wakereketwa wa Bw Odinga walipoanza kulalamika hadharani, rais alichukua hatua za kumtuliza, huku mshauri wake wa masuala ya siasa, David Murathe akisisitiza kuwa Bw Odinga angali chaguo la Ikulu kumrithi Rais Kenyatta hapo 2022.

Baadhi ya wafuasi wa Bw Odinga wana wasiwasi kuwa Rais Kenyatta anajaribu kumchezesha dhidi ya waliokuwa washirika wake kwenye muungano wa National Super Alliance (Nasa).

Muungano huo sasa umechipuka upya chini ya mwavuli wa One Kenya Alliance.

Mudavadi, Musyoka and Wetangula walikuwa pamoja na Bw Odinga chini ya Nasa kwenye uchaguzi wa 2017, naye Bw Moi alikuwa nyuma ya Rais Kenyatta.

Kundi hilo sasa linaonekana kulenga kumtenga Bw Odinga kabla ya uchaguzi wa 2022 likiwa na machungu kuwa aliingia handisheki na Rais Kenyatta mnamo 2018 bila kuwahusisha.

Mbunge wa ODM aliyezungumza na Taifa Leo alisema kuwa kuwa hawamwelewi tena Rais Kenyatta, kwani vitendo vyake vinaonyesha kuwa anamhujumu Bw Odinga.

“Vitendo vya rais vinaonyesha nia mbaya na anatukanganya,” akasema mbunge huyo aliyeomba tusitaje jina lake.

Wabunge hao wa ODM wanahisi kusalitiwa kwa kinara wao licha ya kuwa mwaminifu kwake tangu 2018 walipoingia handisheki.

Ijumaa iliyopita Rais Kenyatta alihudhuria mkutano wa One Kenya Alliance nyumbani kwa mmoja wa vinara wake, siku chache tu baada ya kumtembelea nyumbani kwake Karen jijini Nairobi.

Kabla ya mkutano huo wa One Kenya Alliance, rais alifanya kikao na aliyekuwa waziri Dkt Mukhisa Kituyi, ambaye pia ametangaza atagombea urais.

Mkutano huo umechukuliwa na wafuasi wa Bw Odinga kama ishara ya usaliti kutoka kwa rais baada ya kumtembelea Bw Odinga, ambaye hakuwa na nguvu kufuatia kuugua Covid-19, na hata akamshawishi waandamane kutembea jijini.

Mbunge wa Suna Mashariki, Junet Mohamed analaumu One Kenya Alliance kwa kile aliambia Taifa Leo kuwa jaribio la kutenganisha Rais Kenyatta na Bw Odinga.

You can share this post!

Wanaoenda kuhiji Mecca kuhitaji cheti cha chanjo

Suluhu aunda kamati ya kuchunguza corona TZ