Habari

Rais awasihi Wakenya waongeze imani kwa Mungu

March 21st, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

RAIS Uhuru Kenyatta Jumamosi ameongoza Wakenya katika maombi ya kitaifa yaliyofanyika katika Ikulu ya Rais jijini Nairobi.

Aidha, maombi hayo ya toba, yamelenga kuiombea nchi na dunia kwa jumla, kufuatia janga hatari la Covid-19 na ambalo limetikisa ulimwengu mzima.

Yalianza dakika chache baada ya saa sita za mchana, ratiba ikitwaliwa na wahubiri wa madhehebu mbalimbali nchini, walioshirikisha taifa na ulimwengu kwa njia ya maombi, toba na mahubiri.

Kinyume na hafla zingine za kitaifa, ambapo viongozi wa serikali na kisiasa hupewa fursa kuhutubu, Rais Kenyatta pekee ndiye amezungumza.

“Leo si siku yangu, ila ni siku yetu kama Wakenya ambayo tumeichagua kuungana tumshukuru Mungu kwa mazuri aliyotutendea, kuomba msamaha kama mtu binafsi na taifa kwa jumla,” amesema Rais Kenyatta, akihimiza Wakenya kumsihi Mungu atushushie neema zake kufuatia magumu ambayo taifa na dunia inapitia ya virusi hatari vya corona.

Kabla kutoa hotuba yake fupi iliyosheheni sala za maombi na toba, kiongozi wa nchi ametambua kuwepo kwa asasi mbalimbali za serikali na viongozi wa kisiasa, pamoja na miungano ya kutetea wafanyakazi nchini na jamii ya kibiashara, sekta ambazo zimeathiriwa pakubwa na maambukizi ya Covid – 19.

Kufikia sasa, Kenya imethibitisha visa saba vya virusi vya corona. Kuanzia sekta ya biashara, uchukuzi na hata huduma za serikali kwa umma, zote zimetatizika kwa kiasi kikuu kwa hofu ya maambukizi ya virusi hivyo.

Licha ya juhudi za serikali kupitia idara husika kujaribu kudhibiti maenezi zaidi, Rais Kenyatta ameeleza haja ya wananchi kusimama kidete kwa njia ya maombi “na ninaamini Mungu atayasikial.”

“Kuna wanaosema tunategemea Sayansi, lakini hata Wanasayansi hao wanamtegemea Mungu. Kenya ni nchi inayoamini kwa njia ya maombi, kwa mujibu wa utambulisho wa wimbo wetu wa kitaifa. Ninasihi kila Mkenya aombee uponyaji, umoja na utangamano wa nchi,” amefafanua Rais.

Kilele cha hafla hiyo iliyopeperushwa moja kwa moja kupitia runinga, kimehitimishwa kwa wimbo wa taifa, kifungu cha kwanza, uliokaririwa kwa lugha ya Kiswahili.