HabariSiasa

Rais azuia ziara ya Ruto Mlima Kenya

November 11th, 2019 2 min read

Na NDUNGU GACHANE

HATUA ya Rais Uhuru Kenyatta kufutilia mbali ziara yake katika Kaunti ya Murang’a dakika za mwisho Jumapili iliibua maswali mengi, huku baadhi ya viongozi wakipuuzilia mbali sababu zilizotolewa na Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i aliyetumwa kumwakilisha.

Mbunge kutoka eneo hilo alisema ziara iliyopangwa na Rais ilifanya naibu wake, Dkt William Ruto kufutilia mbali hafla aliyopanga katika kaunti hiyo hiyo kwa kuwa wangeonekana kuwa washindani wa kisiasa.

Ziara ya Rais ilikuwa imesubiriwa kwa hamu kwani wakazi na viongozi wa Mlima Kenya hulalamika kwamba Rais amewasahau tangu alipoingia mamlakani 2017, na huenda tu maeneo hayo kuhudhuria harusi au mazishi.

Wakazi walikuwa tayari wamewasili katika Kanisa la ACK Dayosisi ya Mlima Kenya Kusini, mapema kuanzia saa moja asubuhi kwani walijua hawangeruhusiwa kuingia baada ya Rais aliyetarajiwa kuhudhuria ibada katika kanisa hilo kufika.

Kufikia saa moja unusu, polisi na walinzi rasmi wa Rais walikuwa wamewasili mahali hapo kuanza kupekuapekua na wengine wakasimama pembe tofauti za kanisa. Baadhi yao walichukua usukani katika mkahawa wa nyama choma ulio karibu.

Maafisa wakuu wa utawala wa serikali katika kaunti hiyo akiwemo Kamishna wa eneo la Kati, Bw Wilfred Nyagwanga, na wakuu wa idara ya kitaifa ya ujasusi pia walikuwepo.

Wanasiasa wakiongozwa na Mbunge wa Maragua Mary Waithira, Peter Kimari (Mathioya), Muturi Kigano (Kangema), Isaac Mwaura (Seneta Maalumu) na Job Weru (Mathira) walikuwa tayari kumlaki Rais.

Lakini ilipotimia saa nne unusu, baadhi ya walinzi wa Rais walianza kuondoka, hali iliyofanya wananchi waliokuwepo waanze kuchanganyikiwa kuhusu kilichokuwa kikiendelea.

Karibu dakika 30 baadaye, magari mawili yaliwasili yakiwa yamebeba Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i, mwenzake wa barabara James Macharia na wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) Joe Mucheru.

Dkt Matiang’i alidai Rais amepokea wageni waliokuja nchini kuhudhuria Kongamano la Kimataifa la Idadi ya Watu na Maendeleo (ICPD) ambalo litaanza hapo kesho Nairobi.

“Mnajua jinsi Rais anavyowaenzi na anavyopenda kuwa nanyi, lakini alikuwa anatarajia wakuu wa mataifa ya nje. Ameahirisha ziara yake lakini atajumuika nanyi kwa ibada katika kanisa hili kabla azindue upanuzi wa barabara ya Kenol-Sagan-Marua mwaka ujao,” akasema.

Hata hivyo, viongozi waliohojiwa na Taifa Leo, ambao waliomba wasitajwe walisema hiyo ni sababu hafifu isiyoaminika.

“Hicho ni kisingizio tu cha kutotaka kututembelea. Alijua mapema sana kutakuwa na wakuu wa nchi za kigeni ambao watazuru nchini. Ninamlaumu kwani alisababisha Naibu Rais kufutilia mbali ziara yake. Inahuzunisha sana,” akasema mmoja wa wabunge.

Wengine walisema kuna uwezekano ziara hiyo ingetilia shaka msimamo wake wa kupinga siasa za mapema kwani ingeonekana kama anashindania nafasi na naibu wake Mlima Kenya.

“Pengine aliona ni vyema asubiri hadi wakati atakujia masuala ya maendeleo pekee,” akasema kiongozi mwingine wa kisiasa.

Dkt Matiang’i aliwasilisha Sh2 milioni kutoka kwa Rais, na kila waziri akatoa mchango wa Sh1 milioni.