Habari Mseto

Rais azuru Kisumu kwa mara ya saba

October 16th, 2019 1 min read

Na WAANDISHI WETU

RAIS Uhuru Kenyatta alizuru Bandari ya Kisumu kwa mara ya saba kukagua ujenzi wake unavyoendelea.

Rais alifanya ziara hiyo ya ghafla Jumanne na ambayo ilikuwa ya kufahamu hatua ambayo imepigwa kwenye ujenzi wa bandari ya kisasa inayojengwa kwa gharama ya Sh3 bilioni.

Duru ziliarifu Taifa Leo kwamba ziara hiyo ilichochewa na masuala ibuka kwenye ujenzi huo ambayo yalisababisha hafla ya kufunguliwa kwa mradi huo iliyofaa kuandaliwa Agosti 15 kuahirishwa.

Msemaji wa Ikulu, Bi Kanze Dena-Mararo hata hivyo alisema kwamba hakukuwa na habari zozote kuhusu ziara hiyo ya kushtukiza na hakutoa ufafanuzi zaidi.

Akiwa ameandamana na maafisa wachache, Rais Kenyatta alikaa kwenye bandari hiyo kwa saa mbili akikagua mambo kadhaa kisha akaondoka na kuandaa mkutano na wanaohusika na ujenzi huo katika Ikulu ya Kisumu.

Usalama ulikuwa umeimarishwa huku mamia ya wananchi waliogundua Rais alikuwa eneo hilo pamoja na wanahabari wakizuiwa kuingia kujionea kilichokuwa kikiendelea.

“Rais alisafiri kwa ndege moja kwa moja kutoka Suswa, Kaunti ya Narok alikokuwa akizindua awamu ya pili ya reli ya kisasa SGR hadi Kisumu,” akasema afisa ambaye hakutaka anukuliwe na vyombo vya habari.

Rais na walioandamana naye walitembelea sehemu kuu ya bandari na Taasisi ya Mafunzo ya Usafiri wa Majini.

Meli

Pia alikagua meli ya kale ya MV Uhuru, ambayo imekarabatiwa na hata imefanyiwa majaribio ziwani na kwa sasa imefika hadi nchi jirani ya Uganda.

Vifaa hitajika pia vilisafirishwa kutoka Mombasa, ishara tosha kwamba matayarisho yanaendelea kukamilika na kupisha ufunguzi wa bandari hiyo kwenye hafla ambayo itaongozwa na Rais Kenyatta, Kinara wa ODM Raila Odinga na marais kutoka mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Taifa Leo imegundua kwamba tatizo kuu ambalo limechelewesha ukamilishaji wa mradi huo ni kero la gugumaji na shughuli ya kuchimba na kuondoa mchanga.