Habari

Rais Kenyatta aamuru asasi za uchunguzi zitumie siku 21 kuchunguza ufisadi Kemsa

August 26th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

RAIS Uhuru Kenyatta amesema uchunguzi wa sakata ya ufisadi wa pesa za kukabiliana na Covid-19 katika Shirika la Serikali la Kusambaza Dawa Nchini (Kemsa) unaendelea.

Kiongozi huyo wa nchi hata hivyo ameagiza asasi husika za uchunguzi kufanya hima katika kuchunguza kashfa hiyo, jinsi shirika la Kemsa lilivyotoa zabuni za zaidi ya Sh100 bilioni ilizopokea Kenya kutoka kwa wafadhili kusaidia katika vita dhidi ya corona nchini.

Aidha, Rais Kenyatta amezipa asasi hizo muda wa siku 21 kufanya uchunguzi na kutoa taarifa.

Kwenye hotuba yake kwa taifa mnamo Jumatano, amesema watakaopatikana na hatia, sheria haitakuwa na budi ila kuchukua mkondo wake.

Rais Kenyatta ameeleza kwamba sheria haitasaza wahusika, licha ya ushawishi wao serikalini, kwenye siasa na pia ukwasi walio nao.

“Kwa sababu ya kilio cha umma, taasisi za uchunguzi zifanye hima kuchunguza sakata ya Kemsa chini ya siku 21,” akaamuru, katika hotuba yake ya 11 tangu Kenya ithibitishe kuwepo kwa ugonjwa wa Covid-19.

“Kufuatia kauli yangu katika vita dhidi ya ufisadi, yeyote atakayepatikana na hatia atawajibika,” Rais Kenyatta akaonya.

Tangu kufichuliwa kwa sakata ya Kemsa kuhusu ufujaji wa pesa na vifaa vya matibabu, vilivyotolewa kama msaada kwa Kenya kusaidia kupambana na janga la Covid-19, wanaharakati, watetezi wa haki za kibinadamu na wananchi wamefanya maandamano maeneo mbalimbali nchini, wakitaka wahusika kukamatwa na kuadhibiwa kisheria.

Mnamo Jumanne, kiongozi wa ODM Raila Odinga alisisitiza kuhusu muafaka wake na Rais Kenyatta, katika vita dhidi ya ufisadi nchini, kufuatia salamu za maridhiano, almaarufu Handisheki.

Bw Raila alisema yeye pamoja na Rais wamejitolea kuhakikisha suala la ufisadi nchini limezikwa katika kaburi la sahau, ambapo wahusika wa ufujaji wa raslimali za umma watabeba mzigo wao wenyewe.

Aidha, kiongozi huyo wa upinzani alipuuzilia mbali madai kuwa chama cha ODM kinahusishwa na kashfa ya Kemsa, akihimiza asasi za uchunguzi kufanya uchunguzi wa kina na kufichua wahusika.

Baadhi ya maafisa wakuu wa Kemsa, akiwemo afisa mkuu mtendaji walisimamishwa kazi kufuatia ubadhirifu huo.