Habari

Rais Kenyatta akagua miradi ya maendeleo Pwani

September 7th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA na PSCU

RAIS Uhuru Kenyatta amefanya ziara ya shughuli nyingi huku akikagua miradi ya maendeleo katika sehemu mbalimbali za Kaunti ya Kwale.

Rais ambaye aliandamana na Mkuu wa Majeshi Jemedari Samson Mwathethe alitembelea eneo la kupakulia samaki la Shimoni ambalo serikali kupitia Halmashauri ya Bandari Nchini (KPA) inapanga kulikarabati na kuwa bandari ya kisasa ya shughuli za uvuvi.

Shughuli ya ukarabati wa eneo hilo, na kuwa bandari kamili ya shughuli za uvuvi ikiwemo ujenzi wa maghala ya kuhifadhia samaki yenye mitambo ya barafu, itakamilika katika kipindi cha miezi minane. Mradi huo utagharimu Sh500 milioni.

Ukarabati huo pia utahusu ujenzi wa afisi mpya za mashirika mbali mbali ya serikali na maeneo ya kutia nanga kwa meli ndogo-ndogo za mizigo.

Akiwahutubia wakazi wa mji huo wa Shimoni maarufu kwa shughuli za uvuvi, Rais alisema bandari hiyo, ikijumuisha muundo msingi wake, itasaidia kuchochea shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.

Alisema kama mojawapo wa juhudi za kuhakikisha wenyeji wananufaika na bandari hiyo ya shughuli za uvuvi, serikali itawafadhili vijana 150 kutoka sehemu hiyo kwenda kusomea ubaharia katika chuo kipya kilichoanzishwa cha Mafunzo ya Masuala ya Majini Cha Bandari.

Baada ya hapo, Rais Kenyatta alizuru mji wa Kibuyuni ambako alikagua ujenzi unaoendelea wa kiwanda cha kitakachokuwa kikitayarisha tani 200 za samaki kwa siku. Kiwanda hicho kinajengwa na mwekezaji mmoja kutoka China.

Mara tu kitakapokamilika, kiwanda hicho cha samaki kitaajiri Wakenya 500 kutoka sehemu hiyo na hivyo kuwa soko kwa wavuvi wa kutoka Kenya, Tanzania, Msumbiji, Somalia na Madagascar.

Vilevile, akiwa huko Kibuyuni, Rais alizuru kiwanda cha kutayarisha kwekwebahari ambao ni mradi wa wanawake wa eneo hilo.

Kundi hilo ambalo linaungwa mkono na serikali linashughulika na ukuzaji na uuzaji katika nchi za kigeni kwekwebahari mbali na kutengeneza sabuni kwa kutumia zao hilo.

Rais aliwahakikishia wakazi wa eneo hilo ambao hutegemea sana uvuvi kujikimu kimaisha, kwamba serikali inajibidiisha kutatua changamoto za uvuvi usio halali ili kuwawezesha wakazi hao kupata mapato zaidi kutokana na biashara yao.

Baada ya kuzuru Kibuyuni, Rais alisafiri kwa ndege hadi Vigurungani katika sehemu ya uwakilishi bunge ya Kinango ambako alikagua ujenzi unaoendelea wa barabara ya kutoka Samburu kupitia Kinango hadi Kwale.

Asilimia 78 ya eneo la barabara hiyo ya kutoka Samburu hadi Kinango imekamilika huku kazi za ujenzi zikitarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2019.

Mara tu itakapokamilika, barabara hiyo itafungua ukanda wa eneo la Kusini mwa Pwani kwa uwekezaji wa kibiashara.

Baada ya kutembelea mradi wa ujenzi wa barabara hiyo, Rais alifanya ziara ya ghafla katika sherehe ya makaribisho nyumbani ya Katibu wa Wizara Bi Safina Kwekwe iliyofanyiwa katika Shule ya Msingi ya Mwangoni.

Bi Kwekwe ni katibu katika Wizara ya Utumishi wa Umma, Vijana na Masuala ya Kijinsia.

Akiwahutubia maelfu ya wakazi waliojawa furaha katika eneo hilo, Rais alisema Bi Kwekwe amedhihirisha kuwa mtumishi wa umma mwenye bidii.

Rais ambaye aliahidi kukarabatiwa kwa shule hiyo ya msingi kwa gharama ya Sh11 milioni, alitoa changamoto kwa wasichana wachanga kutoka eneo hilo kumuenzi Katibu huyo wa Wizara na viongozi mashuhuri wa kike waliobobea hapa nchini Kenya.

“Ninyi wasichana wadogo, tafadhali tieni bidii katika elimu yenu. Tafakari jinsi mnavyoweza kupata nyadhifa za uwaziri na pia kuwa Rais wa kwanza mwanamke,” akasema Rais Kenyatta.