Habari

Rais Kenyatta akariri atastaafu ifikapo mwaka 2022

October 16th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

RAIS Uhuru Kenyatta amekariri Jumatano kwamba atastaafu muhula wake wa pili utakapofika tamati huku akipuuzilia mbali madai kwamba Jopo la Maridhiano (BBI) liliundwa ili kubuni nafasi asalie uongozini.

Baada ya uchaguzi mkuu wa 2017 uliofanyika Agosti 8, 2019, taifa lilipitia mengi, maandamano yaliyosababisha vifo vya watu kadhaa yakishuhudiwa.

Uwaniaji wa kiti chenye hadhi ya juu zaidi nchini – urais, kilichohusisha Mabw Uhuru Kenyatta (Jubilee) na Raila Odinga (Nasa) ulizua joto.

Maji yalizidi unga matokeo ya Agosti 8, 2019, ya urais yalipofutiliwa mbali na mahakama ya juu zaidi, kupitia kesi iliyowasilishwa na Nasa.

Marudio yake yalifanyika Oktoba 26, 2019, japo mgombea wa mrengo wa Nasa ulisusia.

Mwaka 2018, kiongozi wa ODM Raila Odinga mnamo Januari 30, 2019, alijiapisha kama ‘Rais wa Wananchi’.

Joto la kisiasa lililotishia kugawanya taifa hili lilitia kikomo Machi 9 Rais Kenyatta na Odinga walipotia saini mkataba wa kuunganisha Wakenya, kuzika katika kaburi la sahau tofauti zao za kisiasa za tangu jadi, kupitia salamu za heri ‘handshake’ au ‘handisheki’.

Maridhiano kati ya viongozi hao yalijiri na mapendekezo kadhaa, ambapo kamati maalum, BBI, ilibuniwa. Ililenga kuhakikisha uwepo wa umoja na utangamano nchini kuanzia uchaguzi mkuu ujao wa 2022.

Waliteua jopokazi likatwikwa jukumu kuzunguka kote nchini kukusanya mapendekezo na maoni ya Wakenya, kuhusu namna ya kusuluhisha vita vinavyoibuka na kusababisha mazingira tata kila msimu wa uchaguzi.

Masuala tisa yakiwemo ushindani au siasa za kikabila, ukosefu wa maadili ya kitaifa, kutokuwepo kwa ushirikishwaji wa wote serikalini, kuhujumiwa kwa ugatuzi, utovu wa usalama, ufisadi, ukosefu wa haki katika chaguzi, kati ya mengine, yaliorodheshwa.

Jopokazi hilo linaloongozwa na seneta wa Garissa Yusuf Haji, lilitekeleza wajibu wake na ripoti ya pamoja inatarajiwa kutolewa hivi karibuni.

Mengi yamejiri kutokana na salamu za maridhiano kati ya Rais Kenyatta na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, tetesi zikiibuka kuwa BBI inalenga kubuni nafasi zaidi za uongozi.

Kwa upande wake Bw Odinga na wanasiasa wanaounga BBI wanahisi kupanuliwa kwa kitengo cha uongozi, ni suluhu kutatua migogoro inayoibuka kila msimu wa uchaguzi.

Wandani wa Naibu Rais William Ruto wanadai BBI ni njama ya kumfungia nje kumrithi Rais Kenyatta mwaka 2022.

Wanasiasa wanaohusishwa na mrengo unaomuunga Dkt Ruto, ‘Tangatanga’, wamekuwa wakikosoa handisheki naye Naibu Rais akiweka wazi kuwa endapo ripoti ya jopokazi itapendekeza kubuniwa kwa nafasi zaidi za uongozi ni suala ambalo halitawezekana.

Kusuta ODM

Ruto amekuwa akisuta chama cha ODM kuwa kinashinikiza kubuniwa kwa nafasi hizo, akitaja hatua hiyo kama yenye tamaa na ubinafsi. Ili hilo kuafikiwa, lazima kura ya maoni kurekebisha katiba iandaliwa, Naibu Rais akisema itarambishwa sakafu.

Naye kiongozi wa muungano wa kutetea wafanyakazi nchini, Cotu Francis Atwoli amekuwa akisema kwamba Rais Kenyatta ni ‘mdogo’ kuondoka uongozini 2022.

Kulingana naye, kubuniwa kwa nafasi zaidi kutamshirikisha serikalini.

Licha ya mengi kusemwa, Rais Kenyatta ameweka wazi kuwa hana haja na nafasi yoyote ile ya kazi akiondoka uongozini 2022.

Kiongozi huyo wa taifa Jumatano amesema ripoti ya BBI inalenga kuunganisha Wakenya.

“Wanasema kuhusu BBI (akimaanisha inapendekeza kubuniwa kwa nafasi za uongozi ili arejee serikalini baada ya 2022), mimi sitaki kazi nimechoka. BBI ni ya kuunganisha Wakenya,” akasema Rais, akitilia mkazo umuhimu wa umoja wa utangamano wa taifa.

Rais Kenyatta amesema hayo wakati akizindua ujenzi wa barabara kuu ya moja kwa moja kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) hadi Westlands.

Katika kile kinaonekana kama kushirikisha kiongozi wa ODM Raila Odinga kwenye mikakati yake ya uongozi, Kenyatta alisema watatengeneza barabara hiyo pamoja.

“Hii barabara mimi na ndugu Raila na viongozi wengine tutaitengeneza,” akasema.

Rais alikuwa ameandamana na gavana wa Nairobi Mike Sonko na Dkt Alfred Mutua wa Machakos, miongoni mwa viongozi wengine kutoka kaunti ya Nairobi na Machakos.