Rais Kenyatta akataa kutia saini mswada wa kuumiza waliopata mkopo wa HELB

Rais Kenyatta akataa kutia saini mswada wa kuumiza waliopata mkopo wa HELB

NA CHARLES WASONGA

WAHITIMU kutoka vyuo vikuu ambao walifaidi kwa mkopo kutoka Bodi ya Kutoa Mkopo kwa Elimu ya Juu (HELB) wamepata afueni baada ya Rais Uhuru Kenyatta kukataa kutia saini Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Bodi ya Mkopo wa Elimu ya Juu, 2020.

Rais Kenyatta alikataa kuutia saini mswada huo unaohitaji kwamba wahitimu waanze kulipa mkopo wao mwaka mmoja baada ya kuhitimu, bila kujali kama wamepata ajira au la.

Pia watahitajika kuanza kulipa faida kwa mkopo huo.

“Mswada huo unaifanyia marekebisho sehemu ya 15 ya Sheria ya Helb kuiruhusu bodi hiyo kuanza kuitisha malipo ya mkopo mwaka mmoja au hata mapema,” mswada huo ukasema.

Mswada huo pia unawahitaji wahitimu waliopata ajira ndani ya mwaka mmoja baada ya kukamilisha masomo kuagiza waajiri wao kuanza kuwasilisha malipo ya mkopo, la sivyo watozwe faini.

“Mhitimu ambaye atafeli kutekeleza mahitaji hayo ndani ya muda uliowekwa atakuwa amekosa na anaweza kutozwa faini ya Sh5,000 kila mwezi. Faini hiyo italipwa kwa HELB,” mswada huo unasema.

Rais amekataa kutia saini mswada huo wakati ambapo HELB imelalamika kuwa inakabiliwa na changamoto za kifedha kutokana na idadi kubwa ya wahitimu ambao hawajamaliza kulipa mikopo yao.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Bodi hiyo Charles Ringera alifichukua kuwa jumla ya wanafunzi 75,000 wanakabiliwa na hatari ya kukosa ufadhili kutoka kwao.

Afisa huyo alieleza kuwa jumla ya wanafunzi 107,000 wa zamani wamefeli kulipa mkopo wa karibu jumla ya Sh10 bilioni.

Idadi hiyo ya wanafunzi wa zamani inajumuisha wale ambao walihamia mataifa ya kigeni kusaka ajira ajira na shughuli zingine za kujiletea mapato.

  • Tags

You can share this post!

Okutoyi apigwa breki raundi ya pili tenisi ya Nottingham...

TAHARIRI: Serikali ichunguze wanachofanya waliopewa leseni...

T L