Habari

Rais Kenyatta akutana na Rais wa Somalia

September 26th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

RAIS wa Misri Abdel Fattah El-Sisi alipanga mkutano wa Jumanne kati ya Rais Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed licha ya uhasama uliopo baina ya mataifa hayo jirani.

Kenya na Somalia zinazozana kuhusu umiliki wa rasilimali ya mafuta na gesi katika mpaka wao ulioko katika Bahari Hindi.

Kila moja inadai kuwa utajiri huo uko ndani ya himaya yake.

Mzozo huo, ambayo ulipelekea Kenya kufurusha balozi wa Somalia nchini, sasa unashughulikia na Mahakama ya Kimataifa kuhusu Haki (ICJ).

Rais Kenyatta alikutana na kufanya mashauriano na Mohamed pembezoni mwa kikao kinachoendelea cha 74 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) jijini New York, Amerika.

Kiongozi wa taifa pia alikutana na Rais wa Djibouti Ismail Omar Guelleh.

“Rais Uhuru Kenyatta jana (Jumanne) jioni alifanya vikao mbali mbali vya mikutano na wenzake wa Somalia na Djibouti Marais Mohamed Abdullahi Mohamed na Ismail Omar Guelleh, mtawalia” taarifa kutoka kitengo cha habari za rais (PSCU) ilisema.

Wakati wa mikutano hiyo, viongozi hao walijadili masuala yanayohusu mataifa yao na bara la Afrika kwa jumla.

Rais Kenyatta alimpongeza na kumshukuru Rais El-Sisi kutokana na mikutano hiyo akisema daima Kenya imekuwa ikipigia debe maelewano ya kuhakikisha kuwepo kwa mashauriano katika moyo wa kudumisha mshikamano barani Afrika.

Huku akirejelea mzozo baina ya Kenya na Somalia, kiongozi wa taifa alisisitiza kwamba kama bara, Afrika yapaswa kutafuta suluhisho kwa matatizo ya Kiafrika.