Habari MsetoMichezo

Rais Kenyatta amuomboleza jagina Kadenge

July 7th, 2019 1 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

RAIS Uhuru Kenyatta amemtaja marehemu Joe Kadenge kama kigogo wa michezo na mwanasoka mahiri aliyetumia kipaji chake kikamilifu kuinua sifa ya nchi.

Katika ujumbe wake wa kuwafariji na kuituliza familia, marafiki na jamaa za Kadenge, Rais Kenyatta alimsifu marehemu kwa kuwa mchezaji hodari aliyejitolea kuboresha soka ya Kenya.

“Joe Kadenge alivuma na kuvutia wengi alipokuwa mchezaji. Alikuwa jagina katika mchezo wa soka na pia mfano bora kwa wanamichezo wengine kwa jumla. Tunasikitika kwamba kifo kimetupokonya mtu aliyeiletea nchi yetu sifa kimataifa,” Rais Kenyatta alisema.

Joe Kadenge aliyeaga dunia jana akiwa na umri wa miaka 84 alifariki baada ya kuugua kwa muda mrefu alikuwa mshambuliaji matata wa Abaluhya United (sasa AFC Leopards) na timu ya taifa ya Harambee Stars.

Kauli maarufu ya ‘Kadenge na mpira’ ilitokana na jina lake kwani ndiye aliyekuwa akitajwa sana redioni kutokana na upepetaji wake wa mpira alipokuwa uwanjani.

Miaka miwili iliyopita, Rais Kenyatta akiandamana na Mkewe, Margaret Kenyatta walimtembelea Kadenge nyumbani kwake katika mtaa wa Mariakani kumtakia afueni kabla ya kumuachia Sh2 milioni.

“Joe alikuwa rafiki yangu mkubwa. Alikuwa na mawaidha ya hekima kwangu wakati tulipomtembelea na Mama wa Taifa nyumbani kwake,” Rais Uhuru Kenyatta alikumbuka.

“Ni mtu aliyeipenda nchi hii, alikuwa na maono mazuri kuhusu soka ya Kenya. Tutamkosa sana kwa kweli,” aliongeza Rais.

Joe Kadenge alikuwa mwanasoka shupavu aliyechezea timu ya taifa kwa miaka 14 kabla ya kustaafu 1969.

Baada ya kustaafu, Kadenge alijiunga na kazi ya ukufunzi na usimamizi wa soka kabla ya kuwa kocha wa timu ya taifa kwa mara kadhaa, mara ya mwisho ikiwa 2002.

Rais Kenyatta alimuomba Mwenyezi Mungu aipe familia, marafiki na jamaa zake nguvu kustahimili msiba wakati huu wa majonzi.