Habari Mseto

Rais Kenyatta amwokoa Leonard Mambo Mbotela

November 14th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

HATIMAYE mtangazaji mashuhuri Leonard Mambo Mbotela Jumamosi, Novemba 14, 2020, aliruhusiwa kuondoka Hospitali ya The Nairobi South alikokuwa amezuiliwa kwa kushindwa kulipa bili ya Sh1.1 milioni.

Hii ni baada ya Rais Uhuru Kenyatta kulipa bili hiyo kufuatia wito uliotolewa na familia yake Alhamisi kutaka msaada.

Duru za familia yake zilisema Jumamosi kwamba Rais Kenyatta alilipa Sh1 milioni pesa taslimu kulipia sehemu ya bili hiyo huku Sh105,498.78 zilizosalia zikilipwa na Wakenya wahisani.

“Mbotela sasa ameruhusiwa kuondoka hospitalini na atakuwa akitunzwa nyumbani,” ikasema taarifa ya familia yake.

Meneja wa wafanyakazi katika Hospitali ya The Nairobi Nairobi South Stephen Mutavi juzi alikunuliwa akisema kuwa gwiji huyo wa utangazaji alilazwa hospitalini humo Oktoba 29,2020.

Hata hivyo, Mutavi hakusema wala kutaja ni ugonjwa upi anaougua mwanahabari huyo.

“Mambo Mbotela alifaa kuondoka hospitalini Ijumaa, Novemba 13 kulingana na ripoti ya daktari lakini ana bili ya Sh1.1 milioni ambazo lazima alipe ndiposa aruhusiwe kwenda nyumbani, tutafurahia iwapo wahisani watajitokeza wamsaidie kulipa bili hii,” Mutavi alisema.

Mbotela mwenye umri wa miaka 80 alifanya kazi kama mtangazaji wa redio ya KBC na runinga kwa zaidi ya miaka 50, tangu 1964. Pia amekuwa mtangazaji wa mashuhuri wa kandanda.

Lakini alifahamika zaidi kutokana na kipindi chake cha redio kwa jina “Je, Huu ni Ungwana?” ambacho kimekuwa kikipeperushwa kupitia  KBC.

Mzee Mambo pia amewahi kufanya kazi katika kitengo cha habari za rais nyakati hizo kikijulikana kama; “Presidential Press Service” (PPS) enzi za Rais wa pili, marehemu Daniel Moi.

Mbotela alistaafu kutoka shirika la Utangazaji la KBC mwaka wa 1997 akiwa na cheo cha mwangalizi mkuu wa vipindi vya redio.

Hata baada ya kustaafu aliendelea kusikika redioni akisoma habari kwa kandarasi na kuendesha kipindi chake “Je Huu ni Ungwana?”