Habari

Rais Kenyatta aomboleza kifo cha mtaalamu wa masuala ya dini wa humu nchini John Mbiti

October 8th, 2019 1 min read

Na PSCU

RAIS Uhuru Kenyatta ametuma salamu za pole kwa jamaa, ndugu na marafiki wa msomi, mwandishi na mhubiri wa Kanisa la Angilikana Dkt John Samuel Mbiti.

Dkt Mbiti alifariki Jumapili akiwa na umri wa miaka 87 nchini Uswisi ambako alihudumu kama Profesa wa maswala ya dini katika Chuo Kikuu cha Bern akiwa pia kiongozi wa Kanisa la Angilikana huko Burgodorf.

Katika salamu zake za pole Rais alisema marehemu Mbiti alikuwa msomi mashuhuri wa Kenya na kasisi ambaye alikuwa balozi stadi wa taifa lake huko ughaibuni.

“Tumempoteza Mkenya mashuhuri. Mtu shupavu ambaye alikabili pingamizi zote na kuwa msomi, mwandishi na kasisi aliyepata ufanisi mkuu. Alikuwa kielelezo bora na balozi mwema wa Kenya huko ng’ambo,” amesema Rais Kenyatta.

Dkt Mbiti aliyepokea shahada yake ya uzamifu katika maswala ya filosofia kutoka Chuo Kikuu cha Cambridge nchini Uingereza mwaka wa 1963, alifundisha masuala ya dini na thiolojia katika Chuo Kikuu cha Makerere kati ya mwaka wa 1964 hadi 1974 kabla ya kuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni ya Masuala ya Dini nchini Uswisi.

Marehemu Mbiti aliandika kuhusu mambo mengi; hasa masuala ya filosofia, thiolojia na destruri za Kiafrika na anakumbukwa sana kutokana na kitabu chake cha ‘African Traditions and Philosophy’ kilichochapishwa mwaka wa 1969.

Rais amemuomba Mwenyezi Mungu kuipa jamaa, ndugu na marafiki wa marehemu Mbiti nguvu za kustahimili msiba wa kumpoteza mpendwa wao.