Rais Kenyatta aonya mawaziri wazembe

Rais Kenyatta aonya mawaziri wazembe

Na SAMMY WAWERU

RAIS Uhuru Kenyatta ametoa onyo kali kwa mawaziri wanaosalia afisini badala ya kujituma kutekeleza kazi walioteuliwa kufanya.

Kiongozi huyo wa nchi amesema Jumatano kwamba katika baraza lake la mawaziri hatastahimili waziri au mawaziri wanaosalia ofisini wakijienjoi, badala ya kuenda nyanjani kuhudumia wananchi.

“Mawaziri tokeni afisini muende nyanjani kuhudumia wananchi,” akaagiza Rais Kenyatta.

Rais alitoa amri hiyo wakati akihutubu katika kongamano la wafanyabishara wa Kenya na Tanzania, lililoandaliwa jijini Nairobi kufuatia ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan, nchini.

“Nendeni mashambani, nendeni kule biashara ziko tuboreshe uchumi. Mawaziri, msingoje kuambiwa mfanye kazi. Mjitume, maana kama unasubiri kuambiwa ufanye kazi inamaanisha hupaswi kuwa afisini,” akasema Rais Kenyatta.

Aidha, Rais alitumia jukwaa hilo kuamuru mahindi yaliyokwama katika boda ya Kenya na Tanzania kuruhusiwa kuingia nchini mara moja.

“Waziri (akimaanisha Waziri wa Kilimo, Bw Peter Munya) hayo mahindi yamesalia mpakani kwa muda mrefu, nimekupa wiki mbili pekee, yawe yameondolewa. Hakuna haja wakulima wetu waendelee kuumia,” akaeleza Rais Kenyatta.

Kufuatia sheria na mikakati iliyowekwa kusaidia kuzuia msambao wa Covid-19, shughuli za usafiri na uchukuzi mipakani zimeathirika, wafanyabiashara wa Kenya na Tanzania wakikadiria hasara ya bidhaa kukawia kuruhusiwa kuingia au kutoka.

  • Tags

You can share this post!

Orengo hatatemwa, Raila afafanua

Nafasi ya ukocha katika timu ya Uingereza U-21 yavutia...