Rais Kenyatta atia saini mswada tata wa vyama vya kisiasa

Rais Kenyatta atia saini mswada tata wa vyama vya kisiasa

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta, Alhamisi, Januari 27, 2022, ametia saini Mswada tata wa Mabadiliko ya Sheria za Vyama vya Kisiasa na kuufanya kuwa sheria.

Mswada huo ulipitishwa katika Seneti Jumatano usiku baada ya maseneta wa mrengo wa handisheki kuwalemea wenzao wandani wa Naibu Rais William Ruto na kupitisha mswada huo bila kuufanyia mabadiliko.

Baada ya mjadala mkali uliosheheni malalamishi na pingamizi kutoka kwa maseneta wa muungano mpya wa Kenya Kwanza (unaoshirikisha vyama vya United Democratic Alliance-UDA, ANC na Ford Kenya), maseneta 29 walipiga kura ya kuunga mkono mswada huo huku saba wakipinga.

Mswada huo ulihitaji kupitishwa na angalau maseneta 24 wanaowakilisha kaunti pekee.

Sheria hiyo inaifanyia marekebisho Sheria ya Vyama vya Kisiasa ya 2011 kwa kuingiza sehemu inayotoa nafasi kubuniwa kwa vyama vya muungano. Inaelezea sifa na wajibu wa vyama vya kisiasa huku ikibadili mfumo utakaotumiwa kugawia vyama vya kisiasa fedha kutoka Hazina ya Ustawi wa Vyama vya Kisiasa.

Sheria hiyo pia inaipa mamlaka afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa ya kuidhinisha orodha ya wanachama wa vyama vya kisiasa, kanuni za uteuzi wa wagombeaji viti miongoni mwa masuala mengine yanayolenga kuimarisha usimamizi wa vyama vya kisiasa.

Vile vile, chini ya sheria hiyo ni wanachama ambao majina yao yako kwenye orodha ya vyama vya kisiasa ndio wataruhusiwa kushiriki katika mchujo wa kuteua wawaniaji viti kwa tiketi ya vyama husika.

Kanda na hayo, watu wanaoataka kusajili chama cha kisiasa sharti kwanza wawasilishe taarifa ianyoelekezea itikadi na sera za chama hicho kwa Afisi ya Msajili wa Vyama vya kisiasa.

Vyama vya kisiasa navyo sasa vitahitajika kubuni miungano miezi minne kabla ya uchaguzi mkuu.

Hii ina maana kuwa vuguvugu la Azimio la Umoja, muungano wa One Kenya Alliance (OKA) na muungano mpya wa Kenya Kwanza, watahitajika kuwasilisha hati ya makubaliano kwa Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu kabla au Aprili 9, 2022.

Watetezi wa sheria hiyo wanasema hiyo itakuza demokrasia ndani ya vyama vya kisiasa na taifa kwa ujumla.

Lakini wabunge na maseneta wa mrengo wa Naibu Rais Dkt Ruto wanasiasa kuwa sheria hiyo imejaa sehemu nyingi zinazokwenda kinyume cha Katiba.

Wakiongozwa na Seneta Kipchumba Murkomen na Mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale, wanasiasa hao wameapa kuwasilisha kesi kortini kupinga utekelezaji wa sheria hiyo.

Mswada huo ulitiwa saini na Rais Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi katika hafla fupi iliyohudhuriwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi, mwenzake wa Seneti Kenneth Kusaka, Mwanasheria Mkuu Paul Kihara, Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Amos Kimunya na mwenzake wa Seneti Samuel Poghisio.

  • Tags

You can share this post!

Kampuni yatengeneza rangi za kisasa

VYAMA: Chama cha Kiswahili cha Triple ‘S’ katika shule...

T L