Habari

Rais Kenyatta atoa tani 20 za vyakula kwa Waislamu

May 15th, 2020 1 min read

Na CECIL ODONGO

RAIS Uhuru Kenyatta ameifaa jamii ya Kiislamu wakati huu wa mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa kutoa tani 20 za vyakula.

Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i aliwasilisha shehena lenye vyakula hivyo kwenye kikao na viongozi wa dini ya Kiislamu katika msikiti wa Jamia ambao ni kongwe zaidi Afrika Mashariki na Kati mnamo Jumatano.

“Hii ni tunu kutoka kwa mheshimiwa Rais kwa Waislamu wakati huu wa mfungo wa Ramadhan,” akasema Dkt Matiang’i akitoa msaada huo, kulingana na habari zilizochapishwa kwenye jarida la kila Ijumaa la Waislamu kwa jina Friday Bulletin.

Baraza Kuu la Waislamu (Supkem) kwa ushirikiano na kamati simamizi ya msikiti wa Jamia, zote zitashirikiana kugawa chakula hicho kwa watu na hasa wa kipato cha chini katika jamii hasa wakati huu ambapo janga la virusi vya corona limeathiri pakubwa uchumi wa nchi.

Mwekahazina wa msikiti wa Jamia Profesa Abdulatiff Essajie alipokea vyakula hivyo, na akasema vitatumika kuwasaidia Waislamu ambao mapato yao yameathirika wakati huu wa virusi vya Covid-19.

“Tunamahukuru mheshimiwa Rais na kumhakikishia kwamba msaada wake utafikia watu au jamii lengwa. Janga la corona limeathiri sana maisha na mapato yetu ndiyo maana msaada huu umekuja kwa wakati unaofaa,” akasema Profesa Essajie.

Msimamizi wa mskiti wa jamia Said Abadalla na Mwenyekiti wa Supkem tawi la Nairobi Ali Golicha pia walihudhuria hafla ya kupokea msaada huo.

jjj