Rais Kenyatta atoa wito kwa viongozi kushirikiana kwa manufaa ya Wakenya

Rais Kenyatta atoa wito kwa viongozi kushirikiana kwa manufaa ya Wakenya

PSCU na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta amewataka wanasiasa kushirikiana kwa lengo la kuimarisha maisha ya Wakenya wakati huu ambapo raia wanakabiliwa na changamoto nyingi.

Rais alisema yeye kama kiongozi wa taifa ataendelea kufanya mazungumzo na viongozi wa mirengo yote ya kisiasa kwa lengo la kuhakikisha taifa linasalia thabiti na lenye umoja.

Akiongea Alhamisi katika Ikulu ya Nairobi, katika dhifa ya chakula cha mchana alichoandalia wabunge, Rais Kenyatta pia aliwakumbusha wanasiasa kuendesha kampeni kwa amani.

“Ni matumaini yangu kwamba moyo wa kufanya kazi pamoja ambao tumeanza, tutaendelea kuudumisha hadi wakati wa uchaguzi mkuu. Tunafaa kulenga masuala yanayowahusu Wakenya huku tukipalilia amani na utulivu,” Rais Kenyatta akasema.

Kiongozi wa taifa aliwapongeza wabunge kwa kupitisha miswada muhimu, ambayo alisema, itasaidia kuimarisha uongozi na utoaji wa huduma kwa Wakenya.

“Naomba kuchukua fursa hii kuwashukuru, haswa enyi wabunge kwa kutenga muda wakati wa likizo na kuweza kupitisha mswada wa marekebisho ya sheria za vyama vya kisiasa. Sote tunajua kwamba ilikuwa likizo ngumu wakati wa janga la Covid-19 lakini mlijitokeza kwa wingi kupitisha miswada ambayo italeta manufaa makubwa,” Rais Kenyatta akasema.

Kuhusu mswada huo tata wa marekebisho ya Sheria za Vyama, Rais Kenyatta alisema mswada huo unalenga kuimarisha uongozi nchini.

Alisikitika kuwa kuna baadhi ya wabunge wanaokashifu mswada huo “kwa manufaa yao.”

“Mswada huo unatupa nafasi ya kufanya kazi pamoja licha ya kutoka vyama tofauti na kwa manufaa ya taifa hili la Kenya. Lakini ole wao wanaupinga jinsi walivyopinga BBI hata bila kung’amua manufaa yake,” akaeleza.

Rais Kenyatta alitumia jukwaa hilo kutoa wito kwa maseneta kupitisha mswada huo bila marekebisho “ili kuhakikisha kuwa taifa hili linafaidi kutokana na manufaa yake.”

Dhifa hiyo ya chakula cha mchana pia ilihudhuriwa na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga ambaye alisema kupitishwa kwa Mswada wa mageuzi ya sheria za Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF) kutaiwezesha serikali kutimiza ahadi yake ya kutoa huduma za afya kwa wote.

Bw Odinga ambaye ni kiongozi wa ODM pia alipongeza wabunge kwa kupitisha mswada wa marekebisho ya sheria za vyama vya kisiasa licha ya pingamizi kali kutoka kwa wenzao wa mrengo wa ‘Tangatanga’.

“Katiba na sheria zozote zile hufanyiwa marekebisho kila mara ili kuoana na mahitaji ya nyakati. Hata Katiba ya Amerika imefanyiwa marekebisho mara nyingi zaidi, lengo likiwa ni kuimarisha uongozi. Kwa hivyo, ninawashukuru zaidi kwa kupitisha mswada wa marekebisho ya sheria za vyama wakati ambapo mlikuwa likizoni,” akasema Bw Odinga.

Wengine waliohutubu katika mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na maseneta wa mrengo wa handisheki walikuwa kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Amos Kimunya, mwenzake katika Seneti Samuel Poghisio na Naibu Spika wa Seneti Profesa Margaret Kamar.

You can share this post!

Vitushi katika Onyesho la Pili, Tendo la Pili la Tamthilia...

Itumbi asimulia masaibu yake mikononi mwa watekaji nyara

T L