Habari Mseto

Rais Kenyatta atuma salamu za pole kwa familia ya mbunge wa zamani wa Likoni

August 25th, 2020 1 min read

Na PSCU

RAIS Uhuru Kenyatta ametuma salamu za pole kwa jamaa, ndugu na marafiki wa aliyekuwa Mbunge wa Likoni Masoud Mwahima ambaye alifariki Jumatatu usiku akiwa na umri wa miaka 78.

Katika salamu zake za pole, Rais amemkumbuka Mwahima kuwa kiongozi wa kitaifa, mwerevu na aliyetumia ushupavu wake kushirikisha wananchi mashinani na kwamba alifanya maendeleo.

“Mzee Mwahima alikuwa mtu mwenye moyo mkunjufu, mwerevu, mzee na kiongozi mwenye maono aliyetoa ushauri wa busara na huduma ya kipekee kwa wakaazi wa Mombasa hasa katika eneo bunge lake la Likoni kwa miongo mingi.

“Akiwa mwanasiasa, Mzee Mwahima alikuwa mtetezi mkuu wa miradi ya maendeleo ya kijamii, sifa iliyomwezesha kupanda ngazi kwenye siasa za Mombasa baada kuhudumu kama diwani, Meya wa Mombasa na baadaye kuwa mbunge wa Likoni kwa mihula miwili,” amesema Rais.

Mwahima alihudumu kama Naibu wa Meya na baadaye kuwa Meya wa Mombasa kuanzia mwaka 1999 hadi 2002 kabla ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa Likoni mwaka 2007, wadhifa alioushikilia kwa mihula miwili. Awali alikuwa diwani wa wadi ya Shika Adabu na Mwenyekiti wa tawi la chama cha Kanu huko Likoni.

Rais aliitakia familia ya mheshimiwa Mwahima na watu wa Likoni faraja ya Mwenyezi Mungu huku wanapoomboleza kifo cha mzee huyo ambaye pia ni kiongozi wa muda mrefu.