Rais Kenyatta aungana na viongozi wengine Dodoma kumuenzi Dkt Magufuli

Rais Kenyatta aungana na viongozi wengine Dodoma kumuenzi Dkt Magufuli

SAMMY WAWERU na CHARLES WASONGA

MWILI wa Rais wa tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Joseph Magufuli umewasili katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma ili kuagwa na viongozi na wananchi.

Leo Jumatatu ni siku ya tatu mfululizo raia wa nchi hiyo kutazama mwili na kumpa heshima za mwisho.

Jumapili, mamia ya maelfu ya Watanzania walipata fursa ya kuuona mwili wa Hayati Dkt Magufuli katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kabla kupelekwa Ikulu ya Chamwino, Dodoma.

Huku maelfu ya raia wa taifa hilo wakijitokeza kumuaga, mwili wake umetolewa Ikulu ukapelekwa Bungeni, kabla kuzungushwa katika afisi za CCM na katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma ambako macho yote yameelekezwa.

Tayari Rais mpya wa Tanzania, Bi Samia Suluhu Hassan amewasili.

Bi Samia alikuwa Makamu wa Rais wa Dkt Magufuli.

Baadhi ya viongozi wa mataifa jirani na mengine ya kigeni pia wanatarajiwa kuungana na Tanzania kumuaga.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ameungana na viongozi wengine jijini Dodoma, Tanzania katika hafla ya kumuenzi Rais wa awamu ya tano Dkt John Pombe Joseph Magufuli ambaye serikali ya nchi hiyo ilisema alifariki Machi 17, 2021, baada ya kuugua. Mama Samia Suluhu alisema alifariki kutokana na tatizo la moyo.

Rais Kenyatta ni miongoni mwa marais tisa na viongozi wa mataifa na wageni wengine mashuhuri waliohudhuria ibada hiyo.

Rais Kenyatta aliandamana na Waziri wa Michezo, Turathi, na Utamaduni Amina Mohamed aliwasili katika uwanja huo wa Uhuru mwendo wa saa nne asubuhi.

Marais wengine waliohudhuria ibada hiyo ni pamoja na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, Lazarus Chakwera (Malawi), Mokgweetsi Masisi (Botswana) na Rais wa Rwanda Paul Kagame.

Wengine ni Rais wa Zambia Edgar Lungu, Emmerson Mnangagwa na Felix Tshisekedi (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC).

Rais Tshisekedi amemtaka Rais Samia Suluhu Hassan na Watanzania kuendeleza ari ya maendeleo aliyokuwa nayo JPM.

“Wimbi la kufariki kwa Dkt Magufuli lisiyumbishe ndoto yenu Watanzania ya kupata mafanikio,” amesema Rais Tshisekedi.

Naye Rais Kenyatta ambaye ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ameanza kwa kumpa pole Rais Samia Suluhu Hassan, mjane Janeth na Watanzania kwa ujumla.

“Kwa Watanzania wote pokeeni pole kutoka kwa EAC na Wakenya,” amesema Rais Kenyatta.

Hotuba ya kiongozi wa Kenya kwa dakika chache iliondolewa kwa vituo vilivyopeperusha hafla hiyo wakati adhana ikisikika kutoka kwa msikiti ulioko karibu.

Gari lililobeba mwili wa Dkt Magufuli wakati likiingia katika uwanja huo, limekuwa na bendera ya Tanzania kumaanisha alikuwa kiongozi wa serikali na vile vile lilikokota mzinga uliolala kumaanisha kwamba taifa la Tanzania linaomboleza na wala sio vita.

Mjane Janeth ameonekana mara kwa mara akitiririkwa na machozi huku akifarijiwa.

Mwili wa marehemu pia utapelekwa Zanzibar na mji wa Mwanza na baadaye kuziKwa nyumbani kwake Chato mnamo Machi 26, 2021.

Magufuli alifanikiwa kupata watoto saba na hadi umauti unamkumba, amekuwa na wajukuu kumi.

You can share this post!

MBWEMBWE: Kante: Shabiki sugu wa tenisi, anachotewa mihela...

Harambee Stars, Mafirauni waingia kambini kabla ya kukabana...