Habari

Rais Kenyatta awaonya wafanyabiashara wakiritimba, wenye tamaa wanaochangia mfumkobei

June 1st, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

RAIS Uhuru Kenyatta Jumamosi amewaonya wafanyabiashara wenye mazoea ya kuongeza bei za bidhaa kiholela hasa za vyakula.

Pia ameagiza Halmashauri ya Bandari nchini (KPA), Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA), Shirika la Kutathmini Ubora wa Bidhaa na Huduma (Kebs) kuacha kuchunguza bidhaa katika bandari zinapoingizwa isipokuwa tu wakati inashukiwa hazijaafiki vigezo vya ubora.

Akionekana kulenga sekta ya kibinafsi, Rais amesema serikali haitakubali kuona wananchi wakiendelea kulemewa na mzigo mzito wa kupanda kwa gharama ya maisha.

Akihutubu katika maadhimisho ya Madaraka Dei 2019 makala ya 56, kiongozi wa taifa amezitaka sekta za kibinafsi kuwajibika na kujali maslahi ya wananchi.

Wanafunzi kutoka shule nane katika Kaunti ya Narok wakifanya wasilisho kuunda ramani ya Kenya na neno Madaraka Juni 1 2019. Picha/ George Sayagie

Amesema baadhi ya sekta za kibinafsi ‘huficha’ bidhaa kama vyakula na kusababisha upungufu ili waongeze bei.

Mfumukobei wa bidhaa ni suala ambalo husababisha kupanda kwa gharama ya maisha.

“Sekta za kibinafsi, ninawasihi mjali maisha ya wananchi. Hii tabia ya kuficha bidhaa hasa vyakula na kuongeza bei ifikie kikomo,” akasema Rais.

Akaongeza: “Kuanzia sasa na kuendelea tutakuwa tukifuatilia bei ya bidhaa nchini.”

Kauli ya kiongozi huyu wa taifa imejiri wakati ambapo Wakenya wanaendelea kufukua mfukoni zaidi ili kugharamia unga wa mahindi.

Mkuu wa Majeshi, Samson Mwathethe alipokagua uwanja wa Narok mwishoni mwa Mei 2019 tayari kwa siku ya siku ambayo ni Juni 1, 2019. Picha/ Maktaba

Pakiti moja ya kilo mbili inauzwa zaidi ya Sh110.

Licha ya Kenya kuwa mkuzaji mkuu wa mahindi, wasagaji wanasema kuwa kuna upungufu wa nafaka hii. Baadhi ya wakulima eneo la Bonde la Ufa wanalalamikia mahindi yao kuozea kwenye maghala, jambo linalosababishwa na bei duni ya bidhaa hii.

Sherehe mashinani

Naye Naibu Rais Dkt William Ruto amesifu hatua ya sherehe za maadhimisho ya sikukuu ya Madaraka Dei kufanyika katika kaunti mbalimbali nchini.

Kulingana na Dkt Ruto ni kwamba hii ni njia mojawapo kuunganisha taifa hili, ambalo awali lilikuwa limegawanyika kwa msingi wa kikabila na kisiasa.

Amesema hatua hii itasaidia jitihada za serikali ya Jubilee kuleta pamoja Wakenya.

“Kinyume na miaka ya awali ambapo maadhimisho ya Madaraka Dei yamekuwa yakifanyika jijini Nairobi, serikali ya Jubilee imeibuka na mfumo wa kuyaadhimisha katika kaunti tofauti ili kuunganisha Wakenya,” akasema Dkt Ruto katika maadhimisho ya Madaraka Dei 2019.

Sherehe za mwaka 2019 ni makala ya 56 na zimefanyika katika Kaunti ya Narok kwa maana kwamba viongozi serikalini wameenda huko.

Maadhimisho ya mwaka 2018, yalifanyika katika Kaunti ya Meru.

Kaunti zingine zilizopata fursa ya kuandaa maadhimisho ya kitaifa nchini, Madaraka Dei na Mashujaa Dei tangu serikali ya Jubilee ichukue usukani 2013 ni Nakuru, Kakamega, Nyeri na Machakos.

Sherehe za Madaraka Dei huadhimishwa nchini kila mwaka kama kumbukumbu ya Kenya ilivyopata uhuru wa kujitawala kutoka kwa utawala wa kikoloni.