Habari

Rais Kenyatta kulihutubia taifa akiwa bungeni Novemba 12

November 3rd, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta anatarajiwa kutoa hotuba kuhusu hali ya taifa mbele ya kikao cha pamoja cha Bunge la Kitaifa na la Seneti mnamo Novemba 12, 2020.

Kwenye taarifa kwa wabunge Jumanne alasiri Spika wa Bunge la Kitaifa Justine Muturi alisema alipokea ujumbe kutoka kwa Rais kwamba analenga kutoa Hotuba Kuhusu Hali ya Taifa bungeni mnamo Alhamisi Novemba 12, kulingana na Kipengele cha 132 (1) ya Katiba.

“Ningependa kuwajulisha wabunge kwamba Kikao Maalum cha Bunge kitafanyika mnamo Alhamisi, Novemba 12, 2020, saa nane na nusu alasiri katika Ukumbi wa Bunge la Kitaifa,” Muturi akasema.

Maspika wa mabunge yote mawili wameanzisha matayarisho ya kufanikisha Kikao Maalum cha Mabunge hayo mawili.

Rais huhitajika kutoa hotuba kuhusu hali ya taifa moja kwa moja kila mwaka kuelezea hatua ambayo serikali imechukua kukabiliana na utovu wa usalama miongoni mwa changamoto zingine.

Hotuba ya mwaka huu 2020 itatolewa wakati ambapo taifa linakumbana na changomoto za kiafya, kiuchumi na kijamii kutokana na maambukizi ya Covid-19.

Kufuatia hali hiyo ni wabunge 120 pekee watakaoruhusiwa kuketi katika ukumbi wa Bunge la Kitaifa huku wengine wakitarajiwa kufuatilia shughuli hiyo chini ya mahema na vyumba maalum katika majengo ya bunge.