Habari

Rais Kenyatta anazindua awamu ya 2A ya SGR kutoka Nairobi hadi Naivasha

October 16th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta leo Jumatano anazindua rasmi awamu ya 2A ya Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Nairobi hadi Naivasha pamoja na kuazisha ujenzi wa barabara kuu ya moja kwa moja kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) hadi eneo la Westlands.

Rais atasafiri kwa garimoshi la abiria kutoka Nairobi ambapo atawahutubia wananchi katika vituo vya SGR katika reli hiyo katika maeneo ya Ongata Rongai, Ngong, Kimuka, Mai Mahiu na Suswa.

Kulingana na taarifa iliyotumwa Jumanne jioni na kitengo cha habari za Rais (PSCU) shughuli kuu ya uzinduzi itafanyika katika kituo cha SGR katika eneo la Mai Mahiu.

Mnamo Jumatatu, kaimu mkurugenzi mkuu wa Shirika la Reli Nchini (KR) Philip Mainga alithibitisha kuwa ni huduma ya treni ya kubeba abiria ndio itaanza huku ile ya uchukuzi wa mizigo ikianza “baada ya miezi kadha ijayo.”

Huduma ya uchukuzi wa abiria itategemewa pakubwa kuzalisha mapato ili kuweza kulipia mkopo kutoka China uliotumiwa katika ujenzi wa reli hiyo ya kisasa.

“Huduma hiyo ya uchukuzi wa abiria itapatikana tu katika vituo vinne kati ya 12 katika awamu hiyo ya SGR. Vituo hivyo ni; Ongata Rongai, Ngong, Mai Mahiu na Suswa. Wasafiri wataanza kutumia ruti hiyo Jumatano,” Bw Mainga akasema.

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo mkuu hakutoa maelezo kuhusu nauli, ratiba ya huduma hiyo na siku ambazo abiria wataweza kutumia treni hiyo kutoka Nairobi hadi Naivasha, kando na vituo vingine vya katikati.

Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, kampuni ya China Communication and Construction Company iliyojenga reli hiyo imekuwa ikiendesha safari za majaribio kama sehemu ya maandalizi kwa uzinduzi wa Jumatano.

Shughuli hiyo ilikuwa imepangiwa kufanyika Juni 30, 2019, lakini ikaahirishwa hadi Agosti na kisha Oktoba 16, 2019.

Hali hiyo ilisemekana kuchangiwa na mvutano uliokuwepo kati ya KR na watu ambao vipande vyao vya ardhi vitatwaliwa kwa ujenzi wa mradi huo, kuhusu fidia.

Wakati huo huo, Rais Kenyatta pia atazindua ujenzi wa barabara kuu (Expressway) ya moja kwa moja kutoka uwanja wa kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) hadi Westlands.

Na mwishowe, atazindua ujenzi wa Depo ya Makasha/Makontena mjini Naivasha (Naivasha Inland Container Depot).