Rais Kenyetta amsimamisha kazi Jaji Chitembwe

Rais Kenyetta amsimamisha kazi Jaji Chitembwe

NA CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta amemsimamisha kazi Jaji wa Mahakama Kuu Said Juma Chitembwe na kubuni jopo la kuchunguza madai kuwa alishiriki ufisadi kinyume na maadili ya afisi anayoshikilia.

Kupitia tangazo kwenye toleo maalum la gazeti rasmi la serikali la Mei 18, 2022 Rais Kenyatta alisema hatua hiyo inafuatia mapendekezo ya Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) iliyosema kuwa madai dhidi ya Jaji Chitembwe ni mabaya na yanaweza kuvuruga imani ya Wakenya kwa utendakazi wa Idara ya Mahakama.

“Baada ya kuchunguza ripoti ya Tume ya Huduma za Mahakama na stakabadhi za kuambatanishwa, Rais ameamuru kama ifuatavyo kwamba:

“Mheshimiwa Jaji Said Juma Chitembwe, Jaji wa Mahakama Kuu, amesimamishwa kazi mara moja,” ikasema notisi hiyo.

Jopo hilo ambalo litamchunguza Jaji Chitembwe litaongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufaa Mumbi Ngugi.

Wanachama wengine wa jopo hilo ni Wakili Mkuu Fred Ojiambo, Jaji Bi Abida Ali Aroni, Jaji Nzioka wa Makau, Jaji James Ochieng’ Oduol, Luteni Jenerali Jackson W Ndung’u na Dkt Lydia Nzomo.

Wakili Mkuu Kiragu Kimani aliteuliwa wakili wa jopo hilo huku Jasper Mbiuki na Sarah Yamo wakiwa makatibu.

Makatibu wengine ni Joseph Gitonga Riungu na Edward Omotii Nyang’au.

Mnamo Novemba 22, 2021 JSC ilianzisha uchunguzi dhidi ya Jaji Chitembwe baada ya aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko kutoa video, taarifa za mitandao ya kijamii na kanda zilizomhusisha jaji huyo na ufisadi.

Wakati huo Chitembwe alipuuzilia mbali madai hayo akisema yalichochewa na chuki.

Bw Sonko pia aliitwa na JSC kutoa ushahidi kuhusu video ambazo zilimhusisha Jaji Chitembwe na ufisadi.

Malalamishi mengi yaliwasilishwa mbele ya JSC yakimhusisha jaji huyo na ufisadi.

Ikiwa jopo litampata Jaji Chitembwe na hatia, atafutwa kazi mara moja. Jaji huyu amehudumu kama Jaji katika Mahakama Kuu kwa miaka 21.

You can share this post!

KINYUA BIN KING’ORI: Wawaniaji wenza sasa...

Kituo cha uchinjaji na utayarishaji wa nyama ya kuku...

T L