Rais Magufuli afunga safari yake ya mwisho duniani leo

Rais Magufuli afunga safari yake ya mwisho duniani leo

Na WAANDISHI WETU

DAR ES SALAAM, Tanzania

TANZANIA inaomboleza, lakini kwa wakazi wa eneo la Chato, si maombolezo ya kawaida.

Alhamisi ilikuwa ni mara ya mwisho kwao kuwahi kumwona mwana wao mpendwa, aliyekuwa Rais John Pombe Magufuli, ambaye amepangiwa kuzikwa leo Ijumaa.

Tofauti na ilivyokuwa miezi iliyopita ambapo kila wakati akizuru Chato angesimama barabarani kuwahutubia, wakati huu hangeweza kuzungumza na makumi ya maelfu ya watu ambao walijitokeza kando ya barabara inayoelekea bomani kwake.

Waombolezaji walijaa barabarani wakilia kwa huzuni, wakatandika kanga na wengine kujirusha chini wakigaagaa.

Wengine wao walipeperusha matawi ya miti nao wengine wakaonekana wakipiga magoti kuomba wakiwa wamebeba mabango yaliyo na maandishi ya ‘Shujaa wa Afrika’.

Ni katika eneo hili ambapo rais wa tano wa Tanzania atazikwa leo Ijumaa, siku tisa baada ya kifo chake kilichotokea Machi 17 katika Hospitali ya Mzena iliyo Dar es Salaam.

Kwa kawaida, Chato huwa ni eneo ambalo halina shughuli nyingi. Lakini idadi kubwa ya wageni walianza kuwasili jana tayari kwa maandalizi ya mazishi.

Walitoka kila pembe ya nchi, na wengine wengi hasa viongozi wanatarajiwa kuwasili kutoka nchi za kigeni leo.

Ulinzi uliimarishwa ndani na nje ya uwanja wa Magufuli uliopo kata ya Muungano wilayani Chato ambapo shughuli ya kutoa heshima za mwisho kwa Magufuli iliandaliwa jana.

Tangu alipofariki, mwili wa Magufuli ulizungushwa katika mkoa wa Dar es Salaam, jijini Dodoma, Zanzibar na Mwanza na hatimaye Chato.

Kutakuwa na misa katika Kanisa Katoliki la Chato kabla mazishi yake kufanyika nyumbani kwake. Serikali ya Tanzania ilitangaza leo Ijumaa kuwa ni siku ya mapumziko kitaifa.

Kwingineko, Mbunge wa Kibamba (CCM), Issa Mtemvu na mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori, Alhamisi waliongoza mamia ya waombolezaji katika ibada ya mazishi ya familia ya ndugu watano wanaodaiwa kufariki kwa kukanyagwa katika shughuli ya kuaga mwili wa marehemu Magufuli katika uwanja wa Uhuru mkoani Dar es Salaam.

Ndugu hao wa familia ya Daudi Mtuwa ni Susan Mtuwa na watoto wake wawili Nathan (6) na Natalia (5) pamoja na watoto wengine wawili Cris (11) na Michelle (8) wa shemeji zake Susan walifariki dunia katika shughuli hiyo iliyofanyika Jumapili Machi 21, 2021.

Akizungumza katika maombolezo hayo, Mtemvu amesema kuwa kazi ya Mungu haina makosa na kila kifo kina sababu zake.

“Nitoe pole kwa familia; hatuwezi kulaumu kwa sababu hili ni jambo la bahati mbaya. Kila kifo kinatokea kwa sababu na ndio maana kuna mwingine ataumwa kichwa. Kazi ya Mungu haina makosa,” akasema.

You can share this post!

BI TAIFA MACHI 31, 2021

Covid-19: Muungano wataka kaunti tano zifungwe