Habari za Kitaifa

Rais: Miradi ya nyumba Uasin Gishu kuajiri 40,000

January 9th, 2024 1 min read

NA TITUS OMINDE

ZAIDI ya vijana 40,000 wanatarajiwa kupata ajira kupitia kwa miradi ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu katika Kaunti ya Uasin Gishu, Rais William Ruto ametangaza.

Akihutubu Jumanne katika mitaa ya Kidiwa, Railways City, na Pioneer iliyoko mjini Eldoret ambako alizindua ujenzi wa vitengo vya nyumba za makazi 10,000, Rais Ruto alisisitiza dhamira ya utawala wake kutekeleza ahadi zake za kampeni ya mwaka wa 2022 kwa Wakenya.

Zaidi ya wapangaji 2,000 katika mitaa lengwa walihamishwa na askari wa kaunti ili kutoa nafasi kwa ujenzi wa nyumba hizo.

Rais Ruto alisema mpango huo wa ujenzi wa nyumba za mabilioni ya pesa utafanywa na vibarua kutoka maeneo lengwa kwa ushirikiano na wahandisi, wasanifu wa mijengo, mafundi wa mifereji na mabomba, waashi na maseremala miongoni mwa wataalamu wengine.

Kiongozi wa taifa alisema tayari vijana 600 wameajiriwa katika awamu ya kwanza ya mradi huo katika mtaa wa Kidiwa.

Kwa muujibu wa rais, ni kwamba idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka na kubuni nafasi za ajira kwa vijana 1,500 kwa kipindi cha miezi miwili ijayo.

“Tunatekeleza mpango wa kuhakikisha Wakenya wanapata makazi jinsi ambavyo Kenya Kwanza iliahidi. Ahadi hii ilikuwa mojawapo ya ajenda yetu kuu ya maendeleo ambayo tuliahidi Wakenya wakati wa kampeni. Tuliahidi ajira na makazi bora kwa mama mboga. Na wakati umefika wa kutimiza,” akasema Rais Ruto.

Rais alisema “sitadhulumiwa na watu wachache wenye ubinafsi na ambao wanatumia mahakama kusitisha ujenzi wa miradi ya nyumba za bei nafuu ambayo inalenga kutengeneza ajira kwa vijana kote nchini”.

Msimamo wa Rais uliungwa mkono na Naibu Rais Rigathi Gachagua ambaye alitilia mkazo kuwa ajenda ya Kenya Kwanza itaendelea bila kuyumbishwa na aliodai ni maadui wa miradi ya maendeleo.

“Rais, ni lazima tutimize ajenda zote ambazo tuliahidi wapigakura wakati wa kampeni bila kuyumbishwa na wachache ambao hawakuwa na imani kuwa tutakuwa uongozini,” alisema Bw Gachagua.