Kimataifa

Rais Mnangagwa alazwa hospitalini Afrika Kusini

May 29th, 2018 1 min read

Na MASHIRIKA

RAIS wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa amelazwa hospitalini kwa “ukaguzi wa kiafya” nchini Afrika Kusini.

Gazeti moja nchini humo liliripoti kwamba kiongozi huyo alipelekwa hospitalini baada ya kupata maumivu yaliyohusiana na chakula cha sumu alichokula mwaka uliopita.

Hata hivyo, duru zilisema kwamba “hayuko hali mahututi.”

“Ataenda nchini Afrika Kusini kwa siku mbili tu na kurejelea majukumu yake. Baada ya kula chakula hicho, madaktari wake walimshauri kwamba lazima awe akikaguliwa mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa hali yake ya afya ni thabiti,” zikasema duru.

Hii ni mara ya pili kwa kiongozi huyo kupelekwa hospitalini kwa dharura tangu kutwaa uongozi mwaka uliopita kutoka kwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Robert Mugabe.