Kimataifa

Rais mpya wa DR Congo augua ghafla akiapishwa

January 25th, 2019 1 min read

NA AFP

RAIS mpya wa DR Congo Felix Tshisekedi Alhamisi aliugua ghafla wakati alipokuwa akiendelea kuapishwa mjini Kinshasa, na kulazimika kusitisha hotuba yake.

Wasaidizi wa Tshisekedi walilazimika kumsaidia kuketi chini baada ya kulalamikia mauvivu akiendelea kusoma hotuba yake muda mfupi baada ya kuapishwa.

“Sijihisi vizuri,” alisikika akisema Rais Tshisekedi kabla ya picha za moja kwa moja za televisheni kuondolewa.

Maafisa wake walionekana wakimhudumia kwa kumpa maji na kumtuliza kuketi.

Baada ya muda mfupi rais huyo mpya alirejea jukwaani na kuendelea kusoma hotuba yake.

“Nafikiri ni uchovu tu wa kipindi kirefu cha kampeni na hisia za hafla hii,” alisema Rais Tshisekedi.

Miongoni mwa viongozi waliofika katika hafla hiyo ni Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Rais wa DR Congo anayeondoka Joseph Kabila pia alihudhuria.

Katika hotuba yake jana kwa taifa, Rais Kabila alisema hajutii chochote na akatoa wito kwa raia wa Congo wamuunge mkono mrithi wake.

Tshisekedi anaingia uongozini wakati sio kila mtu anamuunga mkono kitaifa na hata kimataifa kutokana na kutiliwa shaka matokeo ya uchaguzi mkuu.

Kanisa katoliki lenye ushawishi mkubwa nchini humo lililotuma waangalizi siku ya upigaji kura, linasema data rasmi hailingani na takwimu walizo nazo.

Muungano wa Afrika (AU) uliitaka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo iahirishe kutangaza matokeo ya uchaguzi mkuu.

Muungano huo unaonuia kuhimiza umoja na demokrasia, ulisema una “shaka kubwa” na matokeo ya awali yaliotangazwa wiki iliyopita.

Mgombea mwenzake Martin Fayulu anayedai kuwa ndiye mshindi wa uchaguzi huo, amejitangaza kuwa rais wa pekee wa halali.