Habari Mseto

Rais na familia yake hawana corona – Kanze Dena

June 15th, 2020 1 min read

NA JOHN MUTUA

Maafisa wanne wa Ikulu wamepatikana na virusi vya corona. Msemaji wa Ikulu Kanze Dena alisema kwamba majina ya wanne hao yatabakia siri huku wakitibiwa katika hospitali ya rufaa ya chuo kikuu ya Kenyatta kaunti.

Walipatikana na virusi hivyo baada ya kupimwa wiki iliyopita.

“Katika upimaji uliofanya wiki iliyopita Alhamisi, Juni 11 2020, watu wanne wamepatikana na virusi vya corona  na familia zao na waliotangamana wanashughulikiwa,” alisema Kanze Dena katika ujumbe alioutoa leo.

Alisema kwamba Rais Uhuru na familia yake wako salama na hawana virusi vya corona.

Ikulu imeweka mikakati zaidi kwa maafisa wanaofanya kazi humo na wageni wote ili kuthibiti kusambaa kwa corona.

Haya yanajiri huku maaambuki yakiongezeka kwa visa 133 idadi kamili ikifika 3,727 .

Idadi ya waliofariki imefikia 104 baada ya mtu mmoja kufariki kati ya saa 24.

Watu 1,286 wamethibitishwa kupona virusi hivyo.