Habari MsetoSiasa

Rais, Raila walihofia kuzomewa Kisumu

January 13th, 2020 2 min read

Na RUSHDIE OUDIA

Baadhi ya wakazi katika eneo la Kisumu walipanga kumwaibisha Rais Uhuru Kenyatta wakati wa kuzindua upya bandari jijini humo, hatua iliyopelekea shughuli hiyo kuahirishwa kwa mara nyingine, imefichuka.

Uzinduzi huo ulipangiwa kufanyika kesho lakini ukaaihirishwa kwa mara ya pili huku ripoti, mapema wiki jana, zikiarifu kwamba barua za mwaliko zilikuwa zimetumwa kwa wageni kutoka afisi kuu ya Halmashauri ya Bandari Kenya (KPA) jijini Mombasa.

Wageni hao baadaye waliarifiwa kuhusu kuahirishwa kwa hafla hiyo kupitia barua-pepe iliyotumwa kwa Afisa Mkuu wa Mauzo wa KPA Simon Meja.

“Kuhusiana na mwaliko wa kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa Bandari ya Kisumu na miundomsingi mingine, ningependa kuwaarifu kuwa shughuli hiyo imeahirishwa hadi siku nyingine. Poleni kutokana na mabadiliko haya ya ratiba,” ikasema ujumbe huo.

Kuna ripoti ambazo hazijathibitishwa zilizosema kwamba hafla hiyo iliahirishwa kutokana na hofu ya kiusalama na kutokamilika kwa ujenzi wa baadhi ya sehemu za bandari.

Kwa mujibu wa ripoti fiche kutoka kwa kikosi cha utekelezaji wa maendeleo bandarini, hafla hiyo ilisukumwa mbele kutokana na habari za kijasusi kwamba makundi ya vijana yalikuwa yamepanga kuwaaibisha Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga kwa kuwazoma.

“Wafanyabiashara hasa wa kitengo cha Jua-kali ambao walihamishwa eneo hilo kimabavu wana machungu na hadi leo wanaendelea kuhangaika,” ikaarifa ripoti hiyo.

Aidha, ripoti hiyo ilidai kuwa makundi hayo yalikuwa yakipanga kutumia utata unaozingira kurejea kwa mwanaharakati Miguna Miguna, kujaribu kuzua taharuki jijini Kisumu kabla ya kuwasili kwa Rais na Bw Odinga.

Mnamo Ijumaa wakati wa kikao cha kujadili mapendekezo ya ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) mjini Kisii, Bw Odinga alisema kwamba serikali haiogopi Bw Miguna na anafaa aruhusiwe arejee nchini.

Kabla ya tangazo la kuahirishwa kwa uzinduzi huo, maandalizi yalikuwa yameshika kasi huku maswali yakiibuka kuhusu iwapo marais kutoka mataifa jirani wangefika na kuhudhuria hafla hiyo ya kipekee.

Ingawa siri kali ilidumishwa kuhusu majina ya watu mashuhuri ambao wangefika, kulikuwa na ripoti kwamba Rais wa Uganda Yoweri Museveni na mwenzake wa Tanzania John Pombe Magufuli wangehudhuria.

Mnamo Alhamisi, maafisa wa wizara za Uchukuzi na Miundomsingi wakiongozwa na Katibu katika wizara hiyo Esther Koimett waliandaa mkutano na kuzuru bandari ya Kisumu.

Kulikuwa na mikutano miwili kati ya saa mbili na saa nne asubuhi katika Taasisi ya Mafunzo ya Shirika la Reli ambayo mada yake ilikuwa kujadili namna ya kufanikisha uzinduzi huo.

Mikutano hiyo iliwajumuisha mameneja wa bandari hiyo na shirika la reli, maafisa wa usalama na wenzao kutoka kwa Mamlaka ya Ushuru(KRA).

Kwa mujibu wa afisa mmoja aliyehudhuria, ajenda kuu ilikuwa maandalizi ya mwisho kabla ya uzinduzi uliofaa kufanyika kesho.