Habari za Kitaifa

Rais Ruto avunia Kenya mikataba ya Sh98.8 bilioni ziarani Japan

February 7th, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI

RAIS William Ruto amevunia uchumi wa Kenya mikataba mitamu ya Sh98.8 bilioni katika ziara yake nchini Japan.

Vitita hivyo, kwa mujibu wa taarifa yake rasmi, vitawezesha Kenya kuandaa kituo cha utengenezaji magari mjini Thika kwa ushirikiano wa karibu na wahandisi wa kutoka Japan.

Kampuni ya Toyota Tsusho Corporation ndio itakayoongoza harakati za kuzindua karakana hiyo ya ujenzi wa magari.

Rais Ruto alisema hatua hiyo itafadhiliwa kwa Sh800 milioni katika awamu ya uzinduzi na kuzidishwa katika awamu zitakazofuata.

Alisema Japan pia imejitolea kupiga jeki harakati za kuzindua magari ya kutumia nguvu za umeme badala ya mafuta ya petroli na dizeli.

Aliongeza kuwa mradi huo utawezesha Kenya kupunguza uagizaji wa magari kuukuu na pia uunde nafasi za kazi.

Mikataba mingine ambayo Rais Ruto alijaza kibaba nayo ni pamoja na ule wa Sh75 bilioni wa kuzindua uzalishaji wa nishati kwa kutumia mvuke katika Kaunti ya Nakuru.

Pia kuna mradi wa nguvu za umeme kwa kutumia upepo katika Kaunti ya Meru kwa gharama ya Sh15 bilioni pamoja na ule wa Sh8 bilioni wa kuzalisha umeme kwa kutumia miale ya jua.

[email protected]