Rais Ruto awasilisha ombi la marekebisho ya Katiba kufanikisha baadhi ya mapendekezo ya BBI

Rais Ruto awasilisha ombi la marekebisho ya Katiba kufanikisha baadhi ya mapendekezo ya BBI

NA CHARLES WASONGA

RAIS William Ruto mnamo Ijumaa aliwasilisha memoranda kwa Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula na mwenzake wa Seneti Amason Kingi akipendekeza marekebisho ya Katiba yanayoweza kuchangia kufanyika kwa kura ya maamuzi.

Katika barua yake, Dkt Ruto anapendekeza bunge lianzishe mchakato wa marekebisho ya Katiba ili kubuniwa kwa Afisi ya Kiongozi Rasmi wa Upinzani, kufanikishwa kwa sheria ya usawa bungeni, na kuwekwa kwa sheria ya Hazina ya Ustawi wa Maeneobunge kwenye Katiba (NG-CDF).

Rais pia anataka Hazina ya Usawazishaji (NGAAF) inayosimamiwa na Wabunge Wawakilishi wa Kike kutoka kila Kaunti na Hazina ya Kuchunguza Utendakazi wa Serikali za Kaunti itakayosimamiwa na maseneta, ziwekwe kwenye Katiba.

Kando na hayo, Dkt Ruto pia amewaomba maspika hao wawili kufanikisha marekebisho ya sheria za mabunge hayo ili kuwaruhusu mawaziri wake kufika katika mabunge hayo kujibu maswali moja kwa moja kutoka kwa wawakilishi hao wa wananchi.

Mapendekezo ya marekebisho ya Katiba kubuniwa afisi ya Kiongozi Rasmi wa Upinzani na kuteuliwa kwa wabunge zaidi wa kike ili kufanikisha hitaji la Katiba kwamba angalau thuluthi moja ya wabunge wawe kutoka jinsia tofauti yanagharimu pesa zaidi kwa mlipa ushuru.

Rais pia amependekeza kubuniwa kwa Hazina ya Kuwezesha Wawanawake zaidi kuwania nyadhifa za siasa. Hazina hiyo itabuniwa kutokana na sehemu fulani za fedha ambazo hutengewa vyama vya kisiasa kila mwaka.

Dkt Ruto alisema hazina hiyo itawezesha idadi kubwa ya wanawake kuwania nyadhifa katika chaguzi kuu na hivyo kuzuia hali ya sasa ambapo idadi ya wabunge wa kike haifiki thuluthi moja ya idadi jumla ya wabunge.

“Kwa hivyo, napendekeza kuwa bunge likikubali, Katiba ifanyiwe marekebisho ili kuweka mwongozo wa kubaini idadi ya kila jinsi bungeni kwa misingi ya wabunge waliochaguliwa kutoka maeneo bunge na maseneta waliochaguliwa kutoka kaunti 47 kwa misingi ya vipengele 97 na 98, mtawalia. Marekebisho yanayopendekezwa yanaweza kufanywa katika kipengele cha 97 (3),” Rais Ruto akaongeza katika memoranda hiyo.

Alisema kuna Wabunge wa Kike wawakilishi 47. Idadi inayohitajika kufikia hitaji la angalau thuluthi moja ya wabunge wa kike katika bunge la kitaifa ni wabunge 26 zake. Hii ni kwa sababu wakati huu kuna wabunge 26 waliochaguliwa kutoka maeneo bunge.

Thuluthi moja ya wabunge 290 itakuwa 97.

Katika seneti, kutahitajika kwamba maseneta 14 zaidi wateuliwe ili kufikia hitaji la angalau thuluthi moja yao kuwa wa jinsia ya kike.

Hii ina maana kuwa pendekezo la Rais Ruto likikubalika, wabunge 26 wa kike watateuliwa katika bunge la kitaifa na maseneta 14 zao watateuliwa katika Seneti ili kufikia hitaji la Katiba kwamba angalau thuluthi moja ya wajumbe wawe kutoka jinsia tofauti.

Uteuzi wa wabunge 50 zaidi utapunguza gharama ikilinganishwa na hali ambapo thuluthi moja ya wabunge itakadiriwa kwa misingi ya wabunge 349 na maseneta 67 (wakiwemo wale walioteliwa).

  • Tags

You can share this post!

Kidero agonga mwamba

Masit adai kushurutishwa afuate nyayo za wenzake na ajiuzulu

T L