Rais Ruto kuzuru Pwani tena siasa ikizidi kurindima

Rais Ruto kuzuru Pwani tena siasa ikizidi kurindima

NA WINNIE ATIENO

RAIS William Ruto, anatarajiwa kufanya mikutano Pwani kwa mara ya sita leo Jumatatu wakati ambapo joto la kisiasa limeanza kutanda upya nchini.

Rais amealikwa kufungua rasmi mkutano wa kuwaleta pamoja wabunge wa taifa baada ya Uchaguzi Mkuu, na mkutano mwingine wa viongozi wa mashtaka wa Bara la Afrika.

Ukanda wa Pwani ni mojawapo ya maeneo ambayo yalikuwa ngome kuu ya kisiasa ya kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, akapata ushindani mkali kutoka kwa Dkt Ruto katika Uchaguzi Mkuu uliopita.

Tangu Dkt Ruto alipoingia mamlakani, ukanda wa Pwani umevuna serikalini kwa kupata nafasi za uwaziri, katibu wa wizara, wenyeviti wa mashirika ya kitaifa, uongozi bungeni, na nguvu mpya za utekelezaji miradi mikuu iliyokuwa imeanzishwa wakati wa utawala wa aliyekuwa rais, Bw Uhuru Kenyatta.

Mkutano huo wa wabunge umetokea wakati ambapo mrengo wa Azimio ukiongozwa na kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, umechukua msimamo kwamba hawamtambui Dkt Ruto kama rais.

Hii ni kufuatia ripoti ambayo Bw Odinga anadai ilifichuliwa na mdakuzi kutoka kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), kuonyesha yeye ndiye alishinda katika uchaguzi wa urais.

Kabla Bw Odinga kutoa kauli hiyo, Gavana wa Mombasa, Bw Abdulswamad Nassir, na mwenzake wa Kilifi, Bw Gideon Mung’aro, walikuwa miongoni mwa viongozi wa ODM waliotangaza ushirikiano wa kimaendeleo na Rais Ruto, wakaandamana na rais kwa ziara zake ukanda huo.

Dkt Ruto na viongozi wengine wa mrengo wa Kenya Kwanza, wanatarajiwa kutumia mkutano huo wa wabunge kuhamasisha ushirikiano kati ya afisi ya rais na bunge.

Spika wa Bunge Bw Moses Wetangula alikutana na baadhi ya wabunge ili kujadili kuhusu warsha hiyo.

Kinara wa Mawaziri, Bw Musalia Mudavadi, anatarajiwa kuhutubia wabunge hao kuhusu uhusiano kati ya bunge na afisi ya Rais.

Bw Mudavadi anatarajiwa kutumia mkutano huo kufafanulia wabunge kuhusu majukumu yake serikalini, ikizingatiwa kuwa wizara yake ni ya kipekee.

Vilevile, mkutano huo utatoa fursa wa ufafanuzi kuhusu kama wabunge watakuwa wakimwita Bw Mudavadi bungeni ili kujibu maswali kuhusu serikali ya kitaifa, jinsi ilivyokuwa ikifanywa wakati Bw Odinga alipokuwa Waziri Mkuu katika serikali ya aliyekuwa rais, marehemu Mwai Kibaki.

Wabunge wamekuwa Mombasa tangu wiki iliyopita ambapo walikuwa na kongamano lingine la mafunzo kuhusu shughuli za bunge.

Mkutano wao unaoanza leo Jumatatu, Januari 30, 2023 hadi Februari 2, umefadhiliwa na Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA).

Katika warsha ya viongozi wa mashtaka, mkurugenzi wa kimataifa wa kupambana na dawa za kulevya Kevan Higgins, mkurugenzi wa idara ya kuchunguza uhalifu Amin Mohamed, mkurugenzi wa mashtaka ya umma Noordin Haji na mwenzake wa kulinda mashahidi Bi Jedidah Waruhiu ni miongoni mwa wageni wanaorarajiwa kuhutubia mamia ya wageni.

  • Tags

You can share this post!

Raila akemea Chebukati

Knut yakosoa serikali kurukia Gredi ya 7, 8 na 9

T L