Habari za Kitaifa

Rais Ruto: Mawaziri wote ‘Home’

Na SAMMY WAWERU July 11th, 2024 1 min read

RAIS William Ruto amefuta kazi mawaziri wote wanaohudumu kwenye serikali yake.

Kiongozi wa nchi ametoa tangazo hili muda mfupi uliopita, Alhamisi, Julai 11, 2024 kwenye hotuba yake kwa taifa.

“Chini ya mamlaka niliyopewa na Katiba (akinukuu vifungu), nimefuta kazi mawaziri wote,” akasema Dkt Ruto.

Mwanasheria Mkuu (AG) pia ameangukiwa na shoka la Rais.

Rais Ruto, pamoja na Naibu Rais, Rigathi Gachagua, waliunda Baraza hilo la Mawaziri 2022 baada ya kuchaguliwa Agosti 2022 kama Rais na Naibu Rais, mtawalia.

Kwenye hotuba yake fupi katika Ikulu ya Rais Nairobi, Ruto hata hivyo, alisema Mkuu wa Mawaziri aliye pia Waziri wa Masuala ya Nchi za Kigeni, Musalia Mudavadi hataathirika.

Makatibu hawajaathirika, Ruto akisema utendakazi na huduma za serikali zitaendelea kama kawaida.

Rais Ruto mwaka uliopita, 2023, alinukuliwa akihoji kwamba baadhi ya mawaziri wa serikali yake ya Kenya Kwanza hawana ufahamu wowote kuhusu kazi wanayofanya.

Cha kushangaza, Dkt Ruto alisema yeye ndiye analazimika kuwashauri jinsi ya kuhudumu.

Maamuzi ya Rais kuvunja Baraza la Mawaziri yamechochewa na maandamano ya majuzi ya vijana barobaro, maarufu kama Gen Z.

Dkt Ruto, hata hivyo, hajatangaza siku ambayo atazindua baraza lingine, akiahidi kwamba atashirikiana na Wakenya na wadauhusika wengine kupata mwelekeo.

 

Kaa ange, tutaendelea kukujuza yanayojiri.