Rais Uhuru abadilisha mbinu kuendelea kung’ata Mlimani

Rais Uhuru abadilisha mbinu kuendelea kung’ata Mlimani

Na WANDERI KAMAU

RAIS Uhuru Kenyatta amebuni mbinu mpya kuimarisha usemi wake katika ukanda wa Mlima Kenya, anapojiandaa kung’atuka uongozini mwaka 2022.

Rais Kenyatta sasa anawatumia mawakala kuwafikia wanasiasa waasi, kinyume na awali, ambapo alikuwa akienda moja kwa moja kwa viongozi kuwalaumu kwa kuikosoa serikali yake.

Duru zinasema hilo ndilo limewafanya baadhi ya viongozi ambao walikuwa wakimkosoa kushusha misimamo yao mikali ya kisiasa na kuonyesha dalili za kuanza kumuunga mkono.

Wiki iliyopita, wanasiasa Mwangi Kiunjuri, mbunge Moses Kuria na kiongozi wa Narck-Kenya, Martha Karua, walitangaza mikakati ya kuwaleta pamoja viongozi wa vyama mbalimbali vya kisiasa katika eneo hilo ili “kubuni sauti ya pamoja” ielekeapo 2022.

Bw Kiunjuri ndiye kiongozi wa chama cha The Service Party (TSP) huku Bw Kuria akiongoza Chama Cha Kazi (CCK).Watatu hao walitangaza juhudi za kuwaunganisha viongozi wa zaidi ya vyama 15 katika Ukumbi wa Jumuiya, mjini Limuru, katika kikao kinachoitwa ‘Limuru III.’

Hata hivyo, imeibuka kuwa viongozi hao wameshusha misimamo yao baada ya Rais Kenyatta kuwatuma mawakala wa kisiasa kwao kuwarai “kutathmini mustakabali wa kisiasa wa Mlima Kenya” kutokana na misimamo yao ya kisiasa.Mbali na hayo, imeibuka mawakala hao waliambiwa “kwenda pole pole”, ili kusikiliza malalamishi yote ya viongozi hao.

“Waliambiwa kusikiliza malalamishi yote ya viongozi waasi ili kubuni utaratibu utakaotumiwa kusikiliza malalamishi yao,” zikaeleza duru.Juhudi hizo ndizo zimetajwa kuwashinikiza baadhi ya viongozi kama Bw Kiunjuri na Bw Kuria kuonekana kubadilisha uungwaji mkono wao dhidi ya Naibu Rais William Ruto.

Duru zimeliambia ‘Jamvi la Siasa’ kuwa lengo kuu la Rais Kenyatta ni kuhakikisha eneo hilo limeungana anapojitayarisha kung’atuka uongozini. Inaelezwa ni baada ya kuhakikisha ngome yake imeungana ndipo atakapoanza kumpigia debe kiongozi wa ODM, Raila Odinga kuwa mrithi wake.

“Lengo la Rais Kenyatta ni kuhakikisha anamuuza Bw Odinga katika mazingira tulivu na ambayo hatapata pingamizi kubwa za kisiasa. Hili ni kinyume na ilivyo sasa ambapo eneo hilo limegawanyika vikali, hasa miongoni mwa wanasiasa ambao wamekuwa wakimpigia debe Dkt Ruto,” akaeleza mbunge mmoja ambaye hakutaka kutajwa.

Wadadisi wa siasa wanasema kuwa Rais amechukua mwelekeo huo mpya baada ya kubaini kwamba mbinu yake ya awali kuwakashifu viongozi hadharani ilikuwa ikizua migawanyiko baina yao.

Rais Kenyatta alikuwa akiwakosoa wanasiasa wanaoegemea mrengo wa ‘Tangatanga’ hadharani, akiwaonya “atawafikia hata katika mafichoni mwao.”

Rais ametoa kauli hizo mara kadhaa kwa lugha asili ya Gikuyu, ambako amehojiwa na vituo vya redio vinavyotangaza kwa lugha hiyo.Rais pia alitoa maonyo kama hayo katika vikao viwili ambavyo vimefanyika katika Ikulu Ndogo ya Sagana, Kaunti ya Nyeri, kutathmini mwelekeo wa kisiasa wa ukanda huo.

“Ni wazi kauli za Rais Kenyatta zilizua migawanyiko miongoni mwa viongozi na wafuasi wao. Wanasiasa wa mrengo wa ‘Tangatanga’ walikuwa wakitumia kauli zake kuonyesha jinsi ‘alivyowasahau’ wenyeji wa Mlima Kenya wakilenga kujijenga kisiasa,” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Duru zinasema Rais Kenyatta na washirika wake wamekuwa wakimtumia mbunge Kanini Keega (Kieni) kuwafikia wanasiasa waasi.Inaelezwa hilo ndilo limekuwa likifanya ziara ya kumuuza Bw Odinga Mlima Kenya kuahirishwa kwa mara kadhaa.

Mikakati ya kumpigia debe Bw Odinga katika eneo hilo iliibuka tangu 2019, japo haijawahi kufanyika.Washirika wa karibu wa Rais Kenyatta wamekuwa wakihofia kukabiliwa na pingamizi za kisiasa ambazo zimekuwa zikimwandama Bw Odinga kwa muda mrefu katika eneo hilo.

Mara tu baada ya kuibuka kwa mpango wa kuandaliwa kwa kikao cha Limuru III, Bw Kega aliwashukuru wanasiasa katika ukanda huo, akisema “wameona mwanga.”

“Huu ni mwelekeo wa kuridhisha sana. Ni wazi lazima eneo la Mlima Kenya liwe na sauti moja ielekeapo 2022. Hatuwezi kuruhusu ‘watu kutoka nje’ kutuamulia mwelekeo tutakaofuata. Nawashukuru sana Bw Kuria, Bw Kiunjuri, Bi Karua na viongozi wake wote ambao wameona haja ya Mlima kuzungumza na sauti moja,” akasema Bw Keega.

Wadadisi wanasema mwelekeo huo ndio umemsukuma Bw Odinga kuanza kufanya vikao na mabwanyenye wa kisiaa kutoka Mlima Kenya, wakati Rais Kenyatta anaendelea “kutuliza mazingira ya kisiasa” ili kumpigia debe.

“Wakati juhudi hizo zitafaulu, itakuwa rahisi kumpigia debe Bw Odinga kwani tayari atakuwa amepata uungwaji mkono kutoka kwa mabwanyenye, wanasiasa wenye ushawishi na wenyeji,” asema Bw Oscar Plato, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Hata hivyo, washirika wa Dkt Ruto wanashikilia kuwa hakuna juhudi zozote ambazo zimaweza kuwashinikiza wenyeji wa ukanda huo kumuunga mkono Raila kwani “wamechoshwa na utawala wa Rais Kenyatta.”

“Huwezi kuwalazimisha wananchi kuhusu viongozi watakaowaunga mkono. Wao ndio watajifanyia maamuzi huru,” asema mbunge Rigathi Gachagua (Mathira).

You can share this post!

DINI: Hatuna budi kusali wakati wa mabaya na mazuri tusije...

Kuzimwa kwa BBI kulivyovuruga siasa za urithi 2022