Habari

'Rais ukiwa eneobunge langu jisikie nyumbani'

June 22nd, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

IMEKUWA ni wiki ya ufasaha wa usemi ndani ya mkorogo maalumu ambao ni siasa ndani ya Jubilee na ambapo kilele kilikuwa ni Ijumaa, Rais Uhuru Kenyatta alipoambiwa hadharani ajue ana deni la kubeba naibu wake mwaka 2022.

Hali ilianza Jumapili iliyopita Rais akiwa katika kongamano la imani ya Akorino, alipotoa hotuba iliyojaa makali ya kisiasa akiteta kuhusu wanasiasa wa Jubilee ambao kila uchao wako kiguu na njia kujipigia debe kuhusu uchaguzi mkuu wa 2022.

Katika chama hicho tawala, kuna mrengo wa Naibu Rais, Dkt William Ruto ambao ilionekana Rais aliusuta.

 

Mmoja wa waliokerwa sana na hotuba hiyo ni mbunge wa Kapseret, Oscar Kipchumba Sudi ambaye katika ukurasa wake wa akaunti ya Twitter alionya kuwa Rais Kenyatta amegeuza chama cha Jubilee kuwa mali yake binafsi na ambapo hatambui vyombo vya kufanya maamuzi.

“Wakati mmoja amegeuka kuwa msemaji, mratibu, mwadhibu, mkosoaji, mfanya kesi na mkata kesi, basi hiyo si demokrasia iliyo wazi; ni udikteta,” akaandika Sudi.

Sudi alionya rais Kenyatta kuwa “kuna wengi ambao walijitolea kufa kupona kumpigia debe kwa wapiga kura kiasi kwamba hata wengine walipoteza utajiri na mali katika harakati hizo.”

Alisema kuwa kuna jamii zingine ambazo hazikuwa na nafasi na uwaniaji wake kama Rais “lakini ikawa kunao wa kujitolea kuwa kafara na wakapoteza mengi yao ya maana kumpa ushindi wa awamu ya kwanza ya uchaguzi na kisha ya pili baada ya mahakama ya upeo kubatilisha ushindi wa kwanza.”

Rais akawa amepanga ziara ya kikazi Ijumaa katika eneobunge hilo la Bw Sudi na wengi wakawa wanangojea sasa ‘kieleweke’ na Rais ana kwa ana.

Rais alikuwa ametua kufungua kiwanda cha Rivatex ambacho kilianguka miaka ya tisini (1990s) kutokana na usimamizi mbaya.

Sudi aongea

Sudi akapewa maikrofoni na akawa ndiye huyo amenywea kiasi cha kutangaza kuwa “sisi hatuna Rais mwingine tunayemjua; ni wewe tu.”

“Wewe saa zingine usiwe ukizingatia fitina ndogondogo. Ukiwa hapa elewa kuwa uko nyumbani kabisa,” Sudi akasema.

Lakini mafumbo ya kisiasa yakaingia: “Kile ningetaka ujue tu ni kwamba pale ulipotuacha baada ya kukupigia kura 2013 tuko papo hapo. Sisi ni mzigo wako na wewe ni mzigo wetu lazima tubebane na hakuna kupiga kona hapo katikati; lazima tubebane.”

Hilo likiwa na maana kuwa “tulikupigia kura nasi tunatarajia 2022 tubebane.”

Alimkumbusha Rais kuwa 2013 sio wengi walikuwa wakiamini kuwa Mkikuyu na Mkalenjin wangeshikana pamoja kuwania urais, lakini ikawezekana.

Alimkumbusha Rais kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 “na ndiyo sababu sisi hatuwezi kukubali mtu wa kutuletea fitina ndogondogo…”, hii ikiwa ni njia fiche ya kurushia salamu za maridhiano kati ya Rais na kinara wa upinzani Raila Odinga mshale wa pingamizi.

Alisema kuwa vile rais walishikana na Ruto 2013 “tuko hapo hadi Yesu arudi.”

Alimtaka Rais akichoka Ikulu na presha za mawaziri na wanasiasa, badala ya kulipuka kwa hasira katika hafla za umma, awe akirejea Rift Valley kujipa utulivu wa nyumbani.

Wanasiasa husemwa kuwa ni sawa na mpira kwa kuwa ukishadunda, hujui utaruka kwingine wapi.