Kimataifa

Rais wa Madagascar ajiuzulu ili kugombea urais tena Novemba

September 10th, 2018 1 min read

NA MASHIRIKA

RAIS wa Madagascar Hery Rajaonarimampianina, alijiuzulu Ijumaa kulingana na katiba ya nchi hiyo ili aweze kugombea urais ambao atashindana na kiongozi wa upinzani na aliyekuwa rais Andry Rajoelina.

Rajaonarimampianina alijiuzulu miezi miwili kabla ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Novemba 7 katika kisiwa hicho ambacho kimekumbwa na msukosuko wa kisiasa.

“Wakati umefika kwangu kujiuzulu kulingana na katiba na leo nimewasilisha ombi langu kwa mahakama ya kikatiba,” alisema kwenye hotuba fupi kupitia runinga.

Mwaka huu, raia waliandamana na kumshinikizia Rajaonarimampianina kuunda serikali ya “makubaliano” ya kuandaa uchaguzi.

Waandamanaji walikita kambi katika Central Square jijini Antananarivo kati ya April na Juni kupinga juhudi za Rajaonarimampianina za kubadilisha sheria za uchaguzi. Upinzani ulisema hatua hiyo ilinuiwa kupendelea chama chake.

Mapendekezo hayo yalikataliwa na mahakama. Lakini maandamano hayo yalibadilika kuwa ya kumpindua Rajaonarimampianina.

Watu wawili walikufa kwenye makabiliano kati ya wanaharakati na maafisa wa usalama huku watu zaidi ya 10 wakijeruhiwa.

Mwingine atakayegombea urais ni kiongozi wa upinzani Marc Ravalomanana ambaye alikuwa mtangulizi wa Rajoelina kama rais wa kiraia wa nchi hiyo.

Rajoelina alimwondoa Ravalomanana uongozini kupitia mapinduzi 2009.

Iwapo hakuna mgombeaji atapata asilimia 50 ya kura kwenye awamu ya kwanza, uchaguzi utarudiwa Desemba 19.

Madagascar, ambayo ilikuwa koloni ya Ufaranza ina watu 25 milioni na imekuwa ikikumbwa na misukosuko ya kisiasa iliyosababisha umasikini mkubwa.

Spika wa seneti Riko Rakotovao atakuwa kaimu rais.