Rais wa Masumbwi yasiyo ya malipo duniani kuwasili Kenya Jumamosi

Rais wa Masumbwi yasiyo ya malipo duniani kuwasili Kenya Jumamosi

AYUMBA AYODI na GEOFFREY ANENE

RAIS wa Shirikisho la Ndondi zisizo za malipo duniani (AIBA) Umar Kremlev atawasili nchini Kenya hapo Jumamosi.

Raia huyo wa Urusi mwenye umri wa miaka 38, ambaye alichaguliwa mnamo Desemba 2020, anatarajiwa jijini Nairobi saa saba na nusu mchana.

Atakapowasili, Kremlev, ambaye alipoingia ofisini alisema mipango yake ya kuinua mchezo huo ni pamoja na kuyapa mashirikisho ya kitaifa Sh219.3 milioni kila mwaka, ataelekea katika hoteli ya kifahari ya Kempinski kukutana na maafisa kutoka Wizara ya Michezo, Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki Kenya na Shirikisho la Ndondi za ridhaa Kenya (BFK).

Atakuwa na kikao cha wanahabari baada ya kukutana na maafisa hao kabla ya kuandamana na Rais wa Shirikisho la Ndondi barani Afrika (AFBC) Mohamed Moustahsane kutembelea kambi ya timu ya taifa ya Kenya almaarufu Hit Squad katika ukumbi wa AV Gymnasium.

Hata hivyo, shughuli kubwa ambayo Kremlev amekuja kufanya Kenya ni kuwa na mazungumzo na mataifa wanachama wa AIBA kutoka Afrika kupitia njia ya mtandao mnamo Februari 7, afisa wa mawasiliano wa BFK Duncan “Sugar Ray” Kuria alieleza.

Kongamano hilo litakaloleta pamoja maafisa kutoka bodi ya AIBA na wawakilishi wa mashirikisho ya mataifa litakuwa la kwanza kabisa barani Afrika.

“Litatupa jukwaa la kipekee la mawasiliano kati ya AIBA na mashirikisho ya kitaifa kutoka barani humu. Marais wa mashirikisho ya kitaifa barani Afrika wataweza kupokea majibu kutoka kwa viongozi wa AIBA,” alisema Kuria.

Ajenda nyingine za Kremlev ni kutangaza kamati za AIBA na kalenda ya mashindano, mpango wa kuinua mashirikisho ya kitaifa, mpango wa mawasiliano, warsha za mafunzo ya kukabiliana matumizi ya dawa za kusisimua misuli, ripoti ya kisheria na maswali na majibu.

Kenya ni moja ya mataifa 76 yatakayoshiriki Olimpiki 2020. Itakuwa ikishiriki ndondi kwenye Olimpiki kwa mara yake ya 12 katika makala yajayo mjini Tokyo mwezi Julai/Agosti mwaka 2021.

Nick “Commander” Okoth na Christine Ongare wamefuzu kushiriki mashindano hayo ya haiba, huku Kenya ikitumai mabondia zaidi watajikatia tiketi katika mchujo wa mwisho wa dunia mwezi Juni nchini Ufaransa.

You can share this post!

Historia kuandikwa Mwafrika akiongoza WTO

Biden aahidi kushirikiana na Afrika