Kimataifa

Rais wa Senegal asema nchi hiyo hairuhusu ushoga

February 15th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

DAKAR, SENEGAL

RAIS wa Senegal Macky Sall ametetea hatua ya taifa lake kupiga marufuku mapenzi baina ya watu wa jinsia moja, wakati wa ziara ya Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau.

Mataifa 28 kati ya 49 yaliyoko Kusini mwa janga la Sahara yameweka sheria zinazopiga marufuku shughuli kama vile ushoga na usagaji.

Nchini Senegal watu wanaopatikana na hatia ya kushiriki vitendo kama hivyo hupewa adhabu ya kifungo cha miaka mitano gerezani.

Rais Sall alisema sheria za nchi hiyo zinaoana na mila na tamaduni za watu wake zinazochukulia mapenzi baina ya watu wa jinsia moja kama mwiko.

“Taifa la Senegal haliruhusu mapenzi ya jinsia moja. Sheria zetu sawa na tamaduni za watu wetu hazikubali tabia kama hizi,” Rais Sall akaambia wanahabari jijini Dakar.

Kiongozi huyo alitoa ufafanuzi huo baada ya Waziri Mkuu Trudeau ambaye alikuwa ziarani Senegal baada ya kuzuru Ethiopia, kudai kuwa aliibua suala katika majadiliano kati yao.

“Huwa naibua masuala ya haki za kibinadamu popote ninapoenda. Kila wakati ninapokutana na kiongozi yeyote mimi huzungumzia maadili ya Canada,” Trudeau akawaambia wanahabari.