Kimataifa

Rais wa zamani wa Congo afariki baada ya kuugua corona

March 31st, 2020 1 min read

NA MASHIRIKA

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Congo Jacques Joaquim Yhombi Opango aliaga dunia Jumatatu nchini Ufaransa baada ya kuugua virusi vya corona. Familia yake ilisema alikuwa na umri wa miaka 81.

Mwanasiasa huyo ambaye aliiongoza Congo kuanzia mwaka wa 1977, aliaga dunia akiwa hospitalini jijini Paris, mwanawe alisema.

Yhombi Opango alikuwa mgonjwa kabla ya kuambukizwa virusi ya corona.

Alizaliwa mwaka wa 1939 kaskazini mwa Congo mkoa wa Cuvvette. Alikuwa afisa wa majeshi  na alipanda cheo baada ya mauaji ya Rais Marien Ngouabi.

Aling’olewa mamlakani na mtawala wa miaka mingi Dennis Sassou Nguesso.

Alituhumiwa kushiriki katika njama ya kuipindua serikali ya Sassou Nguesso na kufungwa jela mwaka wa 1987 hadi 1990. Aliachiliwa miezi michache kabla ya mkutano wa kitaifa uliokuwa mwaka wa 1991 ulioleta siasa za vyama mbalimbali nchi zaAfrika Ya kati.

Yhombi ndiye aliazisha Chama cha Demokrasia na Chama cha Maendeleo lakini alipoteza kwenye kura za kuwania kiti cha urais mwaka wa 1992.

Baadaye aliungana na Rais Pasca Lissouba akamchagua kuwa waziri mkuu kuanzia mwaka wa 1994 hadi mwaka wa 1996.

Mwaka wa 1997 alitorokea Ufaransa wakati kuliibuka mapingano nchini humo. Hatimaye alirudi nyumbani mwaka wa 2007.

IMETAFSIRIWA NA FAUSTINE NGILA