Ruto abwaga Raila kuwa rais wa tano wa Kenya

Ruto abwaga Raila kuwa rais wa tano wa Kenya

Katika matokeo yaliyotangazwa Jumatatu jioni na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Dkt Ruto wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) alipata kura 7,176,141 dhidi ya kura 6,942,930 za mpinzani wake wa karibu Bw Raila Odinga wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, hii ikiwa ni tofauti ya kura 233,211.

Kulingana na Bw Chebukati, Dkt Ruto alipata asilimia 50.49 ya kura zote halali zilizopingwa huku Bw Odinga akipata asilimia 48.85.

Dkt Ruto pia alipata zaidi ya asilimia 25 ya kura katika kaunti 39 huku Bw Odinga akipata asilimia sawa katika kaunti 34.

“Kwa mamlaka ambayo nimetwikwa na katiba ya Kenya, mimi Wafula Chebukati, nikiwa msimamizi wa uchaguzi wa urais, ninamtangaza Ruto Samoei William rais mteule wa Kenya kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 9, 2022,” Bw Chebukati alisema huku akishangiliwa na washirika wa Dkt Ruto waliofurika katika ukumbi wa Bomas of Kenya ambapo matokeo yalitangaziwa.

Katika uchaguzi huo, Profesa George Wajackoyah wa chama cha Roots Party aliibuka wa tatu kwa kupata kura 61,969 huku Bw David Mwaure wa chama cha Agano akiwa wa nne wa kura 31,987.

“Huu ndio uchaguzi wangu wa mwisho na nina furaha kuona kwamba tumeufanya kwa njia ya uwazi,” alisema Bw Chebukati.

Dkt Ruto alishukuru Mungu, familia yake, wananchi na washirika wake wa kisiasa kwa ushindi wake na akaahidi wapinzani wake kwamba hawafai kuogopa chochote chini ya utawala wake.

“Najua kwamba ilisemwa kwamba singefika kwenye debe, lakini sasa tuko hapa jioni ya leo. Sio kwa nguvu zetu bali ni kwa nguvu za Mungu,” akasema.

Alisema kwamba katika serikali yake, atatumikia Wakenya wote bila kujali maeneo wanayotoka.

“Huu ni ushindi wa Wakenya na tutaunda serikali ya Wakenya wote. Kila mmoja atahudumiwa na serikali yangu,” alisema.

Alimsifu Bw Chebukati wa kuandaa uchaguzi kwa njia ya haki: “Kama kuna mshindi katika uchaguzi huu, ni IEBC, chini ya Wafula Chebukati ambaye amehakikisha uchaguzi wa hali ya juu ambao kila mtu anaweza kuthibitisha. Kenya inafurahishwa na mikakati ambayo uliweka kuhakikisha kila mmoja anaweza kufuatilia na kuthibitisha matokeo.”

Dkt Ruto alishukuru wapinzani wake kwa kufanya kampeni kwa misingi ya masuala na akawahakikishia kuwa watakuwa na jukumu la kutekeleza la kukosoa serikali yake.

Aidha, Dkt Ruto alimhakikishia Rais Uhuru Kenyatta kwamba hatamwandama akisema amekuwa mshirika wake wa kisiasa kwa miaka mingi: “Ninataka kumshukuru boss wangu, Rais Uhuru Kenyatta ambaye tumejuana kwa miaka mingi. Ninataka kumwambia hafai kuwa na hofu yoyote chini ya serikali yangu. Sina nia kamwe ya kufanya lolote litakalomkosesha amani.”

  • Tags

You can share this post!

Chebukati asimulia mahangaiko yake, maafisa wa IEBC

Jinsi Uhuru alivyosaidia Ruto kuchaguliwa rais wa 5

T L