Michezo

Rakitic apiga bao la pekee Barca ikiilemea Bilbao

June 23rd, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

IVAN Rakitic alifunga bao la pekee na kusaidia Barcelona kusajili ushindi wa 1-0 dhidi ya Athletic Bilbao na kupaa tena hadi kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Barcelona kwa sasa wanajivunia alama 68 kutokana na mechi 31 huku pengo la pointi tatu pekee likitamalaki kati yao na Real ambao wamepiga mechi 30. Chini ya kocha Zinedine Zidane, Real walipangiwa wageni wa Mallorca mnamo Juni 24, 2020.

Rakitic aliingia uwanjani katika kipindi cha pili na kujaza wavuni mpira aliopokezwa na Lionel Messi kunako dakika ya 71.

Hilo lilikuwa bao la 15 kwa Messi kuchangia kambini mwa Barcelona kwenye La Liga msimu huu. Nahodha na fowadi huyo matata mzawa wa Argentina amefungia Barcelona jumla ya mabao 699 kufikia sasa.

Huku Real wakijivunia rekodi nzuri katika mechi zilizowakutanisha na Barcelona msimu huu, Barcelona watasalia kutarajia Real wajikwae katika baadhi ya mechi tisa zilizosalia ndipo wadumishe uhai wa matumaini ya kutetea ufalme wa La Liga muhula huu.

Bilbao walijibwaga ugani kwa minajili ya mechi hiyo ya Juni 23 wakijivunia rekodi ya kushinda Barcelona mara mbili. Kikosi hicho kiliwabwaga Barcelona katika mchuano wa ufunguzi wa kampeni za La Liga msimu huu kabla ya kuwabandua kwenye robo-fainali za Copa del Rey mnamo Novemba 2019.

Messi aliyefikisha umri wa miaka 33 mnamo Juni 24, 2020 alitarajia kupachika wavuni bao lake la 700 wakati wa mechi hiyo dhidi ya Bilbao.

MATOKEO YA LA LIGA (Juni 23):

Barcelona 1-0 Athletic Bilbao

Levante 0-1 Atletico Madrid

Valladolid 1-1 Getafe