Makala

RAMADHANI: Chunguza saum yako ukiwa katika ndoa ya aina hii

June 11th, 2018 2 min read

Na SHEIKH MOHAMED KHALIFA

BAADA ya kumhimidi Mwenyezi Mungu na kumtakia rehema mtume Muhamad (S.A.W), kama tulivyoahidi jana, tunaendelea kujibu maswali kutoka kwa wasomaji wetu walioyatuma kupitia nambari ya ujumbe mfupi 21603.

Tumepokea maswali mawili ya wasomaji ambao japokuwa wamekuwa ndani ya ibada ya mfungo kwa siku ya 26 katika mwezi huu wa Ramadhani, wanatilia shaka kuhusu saum zao, kutokana na hali ya ndoa walizofunga.

Msomaji wa kwanza, ambaye amejitambulisha kuwa Fadhili kutoka Mikindani, Mombasa aliyeoa mke Mkristo anauliza… je ndoa inaweza kufungwa vipi na amekataa katakata kusilimu? Ama kwa dini yetu ya Kiislamu kuishi na mke kama huyu inaruhusiwa? Naomba unifungue tafadhali kwani niko njia panda.

Kwanza tuanze na kauli ya Mtume Muhamad (S.A.W) katika hadithi iliyopokelewa na Anas Bin Malik (R.A) aliyesema, “Mtu anapooa huwa amekamilisha nusu ya dini yake. Basi naazame katika kumwabudu Mwenyezi Mungu ili akamilishe nusu iliyosalia.”

Kwenye kauli hii, dini iliyokuwa ikizungumzia na bwana mtume ni Uislamu. Unaooa mwanamke Mwislamu, ina maana kuwa atakusaidia kuendeleza Usilamu nyumbani mwako. Mama ndiye mwalimu wa kwanza kwa watoto wake na ndiye atakyewafunza yanayohusiana na dini na mengine, hata kabla mtoto hajaanza kuzungumza.

Mwenyezi Mungu (S.W.T) anasema, “Na (mmehalalishiwa kuwaoa) wanawake wema wa Kiislamu na wanawake wema katika wale waliopewa kitabu kabla yenu. (Ni halali kuwaoa) mtakapowapa mahari yao mkafanya nao ndoa bila ya kufanya uzinzi wala kuwaweka vimada….” Sura Al-Maida, aya ya 5.

Waliopewa Kitabu hapa ni Mayahudi waliokuwa na Taurati na Injili. Mwenyezi Mungu hajataja Biblia bali Injili na kwa hivyo ni juu yako kujiuliza kama mke huyo amekataa kuwa Mwislamu, atakusaidia kuwafunza watoto wako Uislamu au la. Pili, mtakuwa mumefunga ndoa kuzingatia dini ipi?

Kwa hivyo ndugu yangu, nakuacha na na maneno ya Mwenyezi Mungu katika Suraatul Dahr inayojulikana pia kama Suratul Al-Insan anaposema, “Kwa hakika tumemuumba mtu kutokana na mbegu ya uhai iliyochanganyika: (ya mwanamume na mwanamke), ill tumfanyie mtihani (kwa amri zetu na makatazo yetu); kwa hivyo tukamfanya ni mwenye kusikia (na) mwenye kuona. Hakika tumembainishia njia (zote mbili hizi; kuwa hii ndiyo ya kheri na hii ndiyo ya shari). Achague kufuata kwa kushukuru au kukufuru, (kukanusha).” (Q76:2-3).

Msomaji wa pili anasema ameishi na mke, wamezaa watoto wanne lakini haajafunga ndoa mbele ya kadhi, japo wazazi wa pande zote mbili wanajuana na hata yeye amelipa mahari. Je, saum yake inafaa?

Nitajibu kwa sentensi moja kuwa maadamu wazazi wameridhia na nyinyi wawili mkakubaliana kisha kukatolewa mahari, hiyo ni ndoa inayotambuliwa na Uislamu.