Makala

RAMADHANI: Dua ya mwenye kufunga hairudi, tujitahidi!

May 24th, 2018 1 min read

Na KHAMIS MOHAMED

DUA ni jambo la lazima kwa kila Muislamu, haswa pindi anapokumbwa na mtihani mzito.

Katika Mwezi huu wa Ramadhani, Allah ni mwepesi sana wa kukubali dua, kwa hiyo Muislamu azidishe zaidi kuomba dua kwani dua ya ndani ya mwezi wa Ramadhan hairudi. Dua ya mwenye kufunga pia hairudi.

Amesema Mtume Muhammad (S.A.W), “Dua ni Ibada. Hakuna ibada tukufu mbele ya Allah kushinda dua.” Dua ni ubongo wa ibada, kwa sababu imekusanya ibada zote; kunyenyekea, kutegemea, kutarajia, kuogopa, kuomba msaada, na kadhalika.

Mwenyezi Mungu (SWT) amesema katika Qurani tukufu (2:186): “Na waja wangu watakapokuuliza juu yangu, basi hakika mimi nipo karibu. Nayaitika maombi ya muombaji anaponiomba, basi waniitikie na waniamini, ili wapate kuongoka.

Aya hii imekuja mara tu baada ya kumalizika kwa aya zinazofaradhisha funga na kuelezea kuhusu mwezi wa Ramadhan.

Hivyo basi, wasomi waliozama katika masuala ya kutafsiri Kuran wanasema kwamba, kuja kwa aya hii baada ya aya zinazohusu funga, ni kuonyesha umuhimu wa mja kuomba dua ndani ya mwezi wa Ramadhan.

Hivyo, tujitahidini sana kuitumia fursa hii iliyotolewa na Muumba Mwenye huruma kwa ajili ya waja wake kujikurubisha karibu naye, kuomba msamaha kwa ajili ya dhambi zao, na kutaka kukidhiwa kwa haja zao.

Amesema Mtume (SAW) katika hadithi Qudsi: “Mwenyezi Mungu asema: Mimi niko pamoja na mja wangu pindi anapoelekea kwangu kwa maombi yake.” (Bukhari na Muslim).

Mwenye kufunga ni miongoni mwa watu watatu ambao wametajwa kuwa dua zao hupokelewa moja kwa moja na Mwenyezi Mungu. Wengine wawili ni msafiri na mtu aliyedhulumiwa.

Na katika hadithi nyingine iliyosimuliwa na Abu Huraira (R.A) na kupokelewa na Ibnu Majah, anasema Mtume (SAW), “Watu watatu dua zao hazirudishwi; Mfungaji mpaka anapofungua, Imamu Muadilifu, na Dua ya mwenye Kudhulumiwa.”