Makala

RAMADHANI: Manufaa chungu nzima kwa mwenye kufunga

May 21st, 2018 2 min read

Na ATHMAN FARSI

NDUGU zangu, nawapeni mkono wa Ramadhani. Naanza na kuwatakieni kila la kheri katika huu mwezi mtukufu ambao huja mara moja kwa mwaka. Mwezi ambao una faida kochokocho. Tutumie nyakati za huu mwezi vizuri sana tusije tukaambulia patupu.

Saum ya Ramadhani ina maana ya kutia nia na kujizuia kula chakula, maji na mambo mengine (chochote ambacho kinabatilisha funga ya muumini) kutoka alfajiri hadi machweo giza linapoingia.

Ni kujizuia kula na kunywa makusudi, kujitapisha, kushiriki ngono ya halali mchana, kusengenya, kutoinamisha macho ya kutizama haramu, kutoenda katika sehemu haramu, kutosikiliza haramu, kutofikiria haramu na kadhalika.

Kufunga kunasaidia siha (afya) na hufanya miili yetu kuyeyusha mafuta mengi yaliyojikusanya kwa miezi 11. Saumu inapoingia husaidia sana mtu kitabia, Imani na huwa kama tiba kwa mwili.

Nyoyo zetu pia hutakasika kwa kuwa na imaani na ustahimilivu wa kimaisha. Waumini hujifunza kuwa watulivu, kujizuia na haramu na pia kujali wenziwao ambao hawajiwezi ikiwemo mayatima. Hali hii huleta muamiliano wa jamii na mujtamaa kwa jumla.

Mwenyezi Mungu ndiye anayejua malipo ya mfungaji, kinyume na ibada nyingine ambazo Waislamu hujua zinalipwaje. Kufunga tukitizama kwa makini kuna faida tele bila hasara ya aina yoyote katika maisha ya mwanadamu.

Allah (s.w.t) ametufaradhishia kufunga ili Muisilamu ajitakase na kumkurubia Mola wake.

Saum inamuokoa mfungaji kutokana na moto wa Jahannam. Mtume wetu (s.a.w) amesema, “Mwenye kufunga siku kwa ajili ya Allah (s.w.t), basi Allah (s.w.t) atamuokoa uso wake kutokana na moto kwa umbali wa miaka sabini” (Muslim)

Mtume Muhammad (SAW) alisema, “Enyi kundi la vijana miongoni mwenu atakae kuwa na uwezo wa kuoa, basi na aoe, kwani kufanya hivyo –kutampelekea- kuinamisha macho yake na kuhifadhi tupu yake; na asiye kuwa na uwezo -wa kuoa- basi ashikamane na funga, kwani hiyo ni kinga kwake”. (Al-Bukhari)

Saum ni sababu ya kupata furaha ya nyumba mbili. Furaha ya kwanza ni mfungaji anapofungua na furaha ya pili ni anapokutana na Mola wake. Bwana Mtume (s.a.w) asema, “Naapa kwa yule ambaye nafsi ya Muhammad iko mikononi Mwake; harufu ya mdomo wa mfungaji ni nzuri mbele ya Allaah kuliko harufu ya miski” (Muslim)

Katika Jannah kuna mlango Rayyan, utakaotumiwa na watu ambao waliofunga tu pekee. Imepokewe hadithi kutoka Al Bukhari kuwa mtume alisema kuwa, “Hakika katika Jannah kuna mlango unaitwa Rayyaan, wataingia humo siku ya Qiyaamah wenye kufunga tu, hatoingia yeyote mwingine, utasema wako wapi wenye kufunga? Watasimama kuingia hatoingia yeyote mwingine, wakishakuingia utafungwa, basi hatoingia mwengine”.

Saumu ni ibaada maalaum ambayo kufuzu kwa maisha kwa Muisilamu kunapatikana ndani yake. Mtume (s.a.w).

“Kila amali njema ya mwanadamu inalipwa mara kumi na inaongezewa thawabu kutoka kumi hadi mia saba; Allah akasema: “Isipokuwa Saum, kwani hiyo ni kwa ajili Yangu na Mimi Ndiye Nitakayemlipa; ameacha matamanio yake na chakula chake na maji yake kwa ajili Yangu.

Kwa aliyefunga atapata furaha mbili; furaha anapofuturu na furaha atakapoonana na Mola wake, harufu inayotoka kinywani mwa aliyefunga ni nzuri mbele ya Allah kuliko harufu ya misk” (Muslim)

Hizi faida tulizozitaja hotofaidika mfungaji yeyote tu kwasababu alifunga kula na kunywa, bali atafaidika mfungaji ambaye alieacha kusema uongo, maneno mabaya, kusengenya, kufitinisha, kutoa ushahidi wa uongo na vitendo vibaya.

La sivyo Allah (s.a.w) hana haja na Saum ya mfungaji ambaye aliacha chakula chake na kinywaji chake bila yakuzingatia mambo yanayo vunja saumu.
Hivyo basi tujitahidi.

 

RAMADHAN
IWAPO una swali au maoni tutumie ujumbe unaoanza na neno SAUM kwa 21603.
Barua pepe ni: [email protected]